Na Said Mwishehe, Michuzi TV

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametangaza kuundwa kwa tume ya watu 14 ambapo saba wanatoka serikalini na saba wanatoka upande wa wafanyabiashara kwa lengo la kushughulikia changamoto zote ambazo zimetajwa na wafanyabiashara nchini.

Majaliwa ametangaza tume hiyo wakati wa kikao kati yake na wafanyabiashara ambacho kilikuwa na lengo la kuzungumza mambo yanayohusu wafanyabiashara sambamba na kuondoa mgomo uliokuwa unaendelea kwa wafanyabiashara wa Kariakoo kwa siku nne mfululizo.

“Kutokana na ombi ambalo limetolewa na wazungumzaji kadhaa kwamba lazima tuwe na tume ya pamoja ili ikae ikumbushane yale ambayo hayakujibiwa leo lakini ili yafanyiwe maboresho hiyo naichukua moja kwa moja na tume nitaisoma hapa.

“Kamati hii itakuwa na watu 14 ambapo kati ya hao saba watoka serikalini na wengine saba kutoka kwenu, nataka nyie muunde timu itakayokwenda kukaa na kutafakari, wawapitishe kwa yale yenu yote yaliyotoka leo na ambayo leo hayakupata nafasi ya kutamkwa hapa

“Ndani ya wiki mbili inatakiwa ipitie na ichukue yote, ianishe yanayotekelezeka leo , kesho hata yale ya sheria na kwasababu Bunge liko bungeni na Waziri atapata mrejesho wa haya na Wizara yake kupitia taasisi yatachakatwa haya na mrejesho mtapewa,”amesema Waziri Mkuu.

Amesema kwa upande wa Serikali wanaoingia kwenye Tume hiyo ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishina wa kodi za ndani TRA pamoja na Kamishina wa sera na Utafiti TRA,

“Tumeunda timu ambayo ikitoka itakuwa na majibu, hakutakuwa tena na swali ,wakishajadili wanarudisha pale.

“Tumekua makatibu wakuu lakini kwa TRA sehemu kubwa ya tozo za ndani ya nchi, kodi, VAT ziko chini ya kamishna wa kodi za ndani kwa hiyo kamishna huyo naye atakuwa kwenye timu hii.Hao ni saba kutoka serikalini.”

Akitaja kwa wawakilishi wa wafanyabiashara ambao wamejumuishwa kwenye tume hiyo ni Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Taifa Bw.Livembe,Mwenyekiti wa soko la Kariakoo Martini Mbwana, mfanyabishara Issa Masoud kutoka Tanga, Fred Vunjabei , Mpandila, Mama Bonge na Omar Hussein kutoka Zanzibar.


Waziri Mkuu ambaye aliwaita wote waliomo kwenye tume hiyo mbele ili wafanyabiashara wawaone amesema amefanya hivyo ili asitokee mtu mwingine akajifanya yeye ni tume akaingia kwenye malalamiko ya hayo wanayolalamikia kuhusu rushwa na akaanza kuomba rushwa huko.

“Kwa hiyo hawa wakija kwenu ndio rasmi naamini mnawaona, watafanya kazi kwenye soko la Kariakoo na masoko mengine ya Jiji la Dar es Salaam, watakwenda Zanzibar , mikoani hasa kwenye majiji kama Mbeya, Mwanza, Arusha, Tanga pamoja na mikoa ya mipani ya Songwe, Kigoma na Mara ili wakutane na wafanyabishara na taasisi za Serikali na wanauwezo wa kumuhoji yoyote ili kupata kitu kitakachoisaidia Serikali.”

Aidha ametumia nafasi hiyo kuwaeleza wafanyabiashara dhamira ya Serikali ni kuona wakifanyabiashara zao na Serikali itaendelea kuwezesha biashara zao na kwamba kilio chao wamekisikia na ndio maana amerudi kuzungumza nao tena kwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Wakati Waziri Mkuu anaanza kuzungumza kwenye kikao hicho pamoja na mambo mengine ameendelea kuwasisitiza moja dhamira ya dhati ya Rais Samia ni kuendeleza sekta ya kibiashara ili kila mtanzania anayeamua kufanya bishara aweze kupata tija ni dhamira ya wazi na ina maelekezo kwao wasaidizi

“Tuyafanyie kazi, tuyasimame na tutoe mrejesho wa mafanikio ,Rais kama Rais rais kama rais ni taasisi kikubwa na ana mana mambo mengi ya kitaifa na kimataifa si kwamba hawezi kuja hapa anaweza kuja ila ni wajibu wetu wasaidizi wake kuja kuanzisha mchakato huu wa kuja na kuwasikiliza.

“Na kwa hiyo basi mwito wenu serikali imeupokea, niliwaomba kibali pale kwamba nimetumwa na Rais kwenda kuzika (Maziko ya Membe)nikirudi tunaanza kikao na leo nimetekeleza nilichoahidi.Kikao kimetoa fursa kwa wengi kuzungumza kwa undani zaidi na kwa uwazi.

“Niwaahidi hatufungi milango kikao hiki leo tunaendelea nayo na mengine tutakwenda nayo mkapa kwenye Baraza la Biashara la Taifa ambako wako viongozi wenu na Mwenyekiti wa baraza hilo ni Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.

“Niwaambie Rais Samia Suluhu Hassan katika kuamini biashara kuwa ndio sekta inayoinua uchumi wa nchii, sekta inayowezesha kila mtanzania anayepata kipato chake aliamua kuunda mabaraza hayo na kuagiza kuanza kufanya maboresho ili wafanyabiashara wadodo, wakati na wakubwa wapate nafasi ya kuzungumza.

“Akafungua milango kwenye sekta ili wawekezaji waje nchini ili kuchangia uchumi wa nchi hii, malengo haya yanawezesha Taifa hili kupata mafanikio na sisi tumepata nafasi ya awali kuingia katika sekta hii ya biashara, Rais wetu ametoa msisitizo wa kuingia kila sekta sasa tuingie kwenye biashara.

“Hivyo basi muwe tayari na mmeanza endeleeni lakini kama umekuja hapa hujaanza biashara , anza biashara fursa ipo na serikali ipo itakutumikia.Nachoweza kueleza hoja zote ambazo zimezungumzwa hapa leo na zile ambazo zilizungumzwa na viongozi wenu tutakuja kuwapa mrejesho,”amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizingumza na wafanyabiashara wa soko la kariakoo, katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam Mei 17, 2023.


Timu ya pamoja kati ya viongozi wa Serikali na wafanyabiashara iliyoundwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambayo itakaa na kupitia changamoto zilizopo katika soko la kimataifa la Kariakoo, katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam Mei 17, 2023. Timu hiyo inajumuisha watu 14.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...