Na Beatus Maganja

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Tanzania kupitia  Sekta ya Utalii imeshuhudia kuvunjwa Kwa rekodi ya idadi ya watalii waliotembelea Nchi Yetu Kwa shughuli mbalimbali za Kitalii wakiwemo watalii wa uwindaji wa kitalii ikiwa ni idadi kubwa kuwahi kuipokea kuliko Wakati wowote katika historia ya kuanzishwa Kwa sekta hiyo.

Ameyasema hayo leo June 2, 2023 akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii Kwa Mwaka wa fedha 2023/2024 Jijini Dodoma ambapo ongezeko hilo ni kwa mujibu wa taarifa za miezi 10 tu yaani kuanzia Julai mwaka jana hadi Aprili mwaka huu.

"Mheshimiwa Spika, pamoja na kuongezeka Kwa ujumla Kwa idadi ya watalii Kitaifa, katika kipindi hiki cha utekelezaji, taasisi kubwa za Utalii Nchini zimeshuhudia kuvunjwa Kwa rekodi ya idadi ya watalii katika maeneo yao..." amesema

"..Kwa Upande wa TAWA watalii wa Uwindaji wameongezeka kutoka 541 Kwa Mwaka 2021/22 hadi kufikia watalii wa uwindaji 692 Kwa kipindi Cha miezi 10 tu ya mwaka wa fedha 2022/23" amesema

Katika jitihada za kuendeleza uhifadhi wa rasilimali muhimu Mhe. Mchengerwa amesema Wizara imefanikiwa kupandisha hadhi Mapori Tengefu mawili (2) yaani Kilombero na Pololeti kuwa Mapori ya Akiba

Aidha amesema hatua hiyo imeongeza idadi ya Mapori ya Akiba Nchini kutoka 27 hadi 29 lengo likiwa ni kuimarisha ulinzi na matumizi endelevu ya rasilimali na utunzaji wa vyanzo vya maji.

Katika kuendeleza jitihada za Kukabiliana na changamoto za migogoro baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu Waziri Mchengerwa ameiagiza TAWA na Wataalamu wengine wa wanyamapori  kuendelea kutoa elimu Kwa wananchi  kuhusu namna ya kujikinga na wanyamapori hao na kuwafundisha askari wa vijiji mbinu zaidi za medani.

Hata hivyo Waziri Mchengerwa amebainisha mikakati 10 ya Wizara yake anayoendelea nayo katika kudhibiti changamoto ya Wanyamapori Wakali na Waharibifu.

Amesema kukamilisha Maelekezo ya Baraza la Mawaziri juu ya Mipaka kati ya vijiji 975 vilivyokuwa na Migogoro na Hifadhi, kuendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa utatuzi wa Migogoro baina ya binadamu na Wanyamapori Wakali na Waharibifu (2020 -2024) na kutoa elimu kuhusu namna ya Kukabiliana na wanyama hao ni sehemu ya mikakati yake.

Mikakati mingine ni pamoja na kutoa vifaa Kwa wananchi vya kupambana au kuwafukuza Wanyamapori Wakali na Waharibifu, kutoa kifuta jasho na machozi Kwa wanaoathirika na Wanyamapori Wakali na Waharibifu pamoja na kufanya utafiti Kwa kuwafunga mikanda ya mawasiliano viongozi wa makundi ya Wanyamapori hao Ili kubaini mienendo yao.

Mingine ni kutumia ndege Maalum kuondoa Wanyamapori kwenye makazi, kuongeza vitendea kazi vya kupambana na Wanyamapori Wakali na Waharibifu, kuongeza Askari wa Doria na kutumia Askari Wanyamapori wa vijiji pamoja na kuunda Kamati Maalum ya Wataalamu kumshauri Waziri. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...