Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Serikali inaendelea na jitihada za kumaliza changamoto ya magugu maji kuzingira Ziwa Jipe wilayani Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro.

Amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mwanga Mhe. Joseph Tadayo aliyetaka kujua lini Serikali itatekeleza mradi wa kuondoa magugu maji katika Ziwa Jipe.

Dkt. Jafo amesema Ofisi hiyo kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) tayari zimefanya tathimini ya uharibifu uliopo na kuandaa andiko la Mradi wa Hifadhi ya Ardhi, na vyanzo vya maji.

Akiendelea kujibu swali hilo amebainisha kuwa jumla ya Dola za Marekani milioni sita ambazo ni sawa na takriban shilingi bilioni 15 zinatarajiwa kupatikana kupitia mradi huo.

“Serikali imeona changamoto ya uharibifu wa Mazingira unaotokana na kuenea kwa magugu maji katika Ziwa Jipe, hadi sasa jitihada za kutafuta fedha kutoka kwa wafadhili mbalimbali zinaendelea,” amesema Mhe. Jafo.

Amefafanua kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha inarejesha ikolojia ya ziwa hilo ili kuleta manufaa kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo pamoja na uhifadhi wa mazingira.

Aidha, Waziri Dkt. Jafo ameongeza kwa kusema kuwa Serikali itahakikisha inatekeleza mradi huo mara baada ya fedha kupatikana ili kuwanusuru wananchi wa eneo dhidi ya athari za magugu maji hayo.

Pamoja na majibu hayo pia Waziri Jafo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuhifadhi mazingira katika Ziwa Jipe ikiwemo kuacha kufanya shughuli za kibinadamu zisizo endelevu.

Ziwa Jipe lina ukubwa wa kilomita za mraba 30 na linahudumia wananchi zaidi ya 3,000 wanajishughulisha na shughuli za uvuvi, kilimo, ufugaji na uhifadhi wa bionuwai pamoja na shughuli za utalii.

Hata hivyo inaelezwa kuwa shughuli za uvuvi zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na kukithiri kwa magugu maji yaliyoota ziwani hasa upande wa Tanzania hivyo Serikali inaendelea na jitihada za kuondoa magugu maji hayo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akijibu maswali bungeni kuhusu hatua za Serikalo katika kudhibiti magugu maji katika Ziwa Jipe, wakati wa Kikao cha tatu Mkutano wa 12 wa Bunge jijini Dodoma leo tarehe 31 Agosti, 2023.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akimfafanulia jambo Mbunge wa Mwanga Mhe. Joseph Tadayo wakati wa Kikao cha tatu Mkutano wa 12 wa Bunge jijini Dodoma leo tarehe 31 Agosti, 2023.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...