Na Mwandishi wetu –Kilimanjaro

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amewatahadhalisha wanawake kutochukua mikopo itakayowarudisha nyuma kimaendeleo maarufu Kausha damu.

Mhe. Ummy ameyasema hayo alipotembelea Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Kilimanjaro zikiwemo Wilaya za Moshi Mjini na Siha na kuzungumza na Baraza la Wanawake la Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na vikundi vya wanawake ambapo amewasihi wanawake kuwa makini pindi wanapoamua kuchukua mikopo hiyo.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ina nia njema ya kuhakikisha kina mama wanajikwamua kiuchumi kupitia asilimia 10% ya mikopo inayotolewa na kila Halmashauri.

“Utaratibu wa mikopo hiyo utakaporejeshwa kina mama wapewe kipaumbele na mfanye shughuli za maendeleo halafu kina mama wa mjini tuache kukopa mikopo ya kausha damu kwasababu ni mibaya wakati mwingine inavunja ndoa kwahiyo kabla ya kukopa omba ushauri usiingie kwenye madeni na kupata fedheha,”Amesema Mhe. Ummy.

Kuhusu Ilani ya Chama Cha Mapinduzi amebainisha kuwa imeendelea kutekelezwa katika sekta mbalimbali kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo huku akitoa onyo kwa baadhi ya watu wasiyo na nia njema na Serikali kuacha kubeza juhudi za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Tuendelee kuungana mkono, tuendelee kukisemea Chama kwasababu ilani ya Chama inatekelezwa vizuri na kazi inaendelea kina mama tutembee kifua mbele kina mama tunaye Mhe. Rais Dkt. Samia jasiri na jemedari anafanya kazi kubwa na nzuri,” Amebainisha Mhe. Ummy.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), Mkoa wa Kilimanjaro Ndug. Elizabeth Minde amewahimiza watanzania kuendelea kuheshimu na kulinda Amani ya Nchi iliyopo kwa kuepuka kutumiwa na baadhi ya watu wasiyo na nia njema na Taifa la Tanzania.

Katika hatua nyingine Mbunge huyo amegawa mitungi ya gesi kwa vikundi vya wanawake Wilaya ya Moshi Mjini na Wilaya ya Siha kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya safi ya kupikia na kuepuka matumizi ya kuni na mkaa ili kuhifadhi mazingira.

“Hatuhitaji Nchi yetu kuingia katika migogoro mikubwa itakayofanya watu wasitulie kutekeleza shughuli za kimaendeleo tunahitaji maendeleo kwa sababu inapotokea migogoro kina mama, watoto, wazee na watu wenye ulemavu ndiyo wanaoathirika zaidi, “ Ameeleza Mwenyekiti huyo.

Aidha Mkuu wa Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro Dkt. Christopher Timbuka amewataka kina mama kupaza sauti zao kupinga vitendo vya ukatili katika jamii na uvunjifu wa maadili badala ya kuwa sehemu ya kuwaficha wanaofanya vitendo hivyo hatua inasababisha kuongeza kwa matukio ya kikatili.

“Wilaya ya Siha inaongoza kwa vitendo vya ukatili na shida kubwa ya Siha ni kufichiana siri wakati tunaamini kina mama ni jeshi kubwa naomba tutoe ushirikiano kuzuia vitendo vya kikatili na mmomonyoko wa maadili kwa kutoa taarifa za wanaofanya vitendo hivyo,”Amehimiza Dkt. Timbuka.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...