Na Mwandishi Wetu, Nzega
MKUU wa Wilaya ya Nzega mkoani Tabora Naitwapwaki Tukai ameweka wazi kwamba atahakikisha anakula sahani moja na mtu akikundi chochote kinachohujumu vyandarua vya Serikali.
Ametoa kauli hiyo wakati wa tukio la usambazaji wa vyandarua unaofanywa na Bohari ya Dawa (MSD) ambapo amesisitiza iwapo atabaini yupo anayeuza au kufugia kuku vyandarua hivyo kwa kisingizio kuwa vinapunguza nguvu za kiume hatamvumilia.
“Nzega inahitaji watu waaminifu hivyo sitamvumilia atakayeuza vyandarua vya Serikali na niwaambie wafanyabiaahara msijaribu nikikuta dukani kwako wewe ni muhujumu, utalipa vile ninavyotaka mimi au kufilisiwa .Vyandarua hivi ni mali ya Serikali."
Aidha amewataka wanawake wasikubali kudanganywa na kukimbiwa kitandani kwani mwanaume hawezi kukosa nguvu kwa kulala katika chandarua chenye dawa."Kama huna nguvu basi huna tu."
Akisisitiza Naitwapwaki amesema hatakubali kuona jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kuboresha maisha ya Watanzania na sekta ya afya yanarudishwa nyuma kwa makusudi.
Amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kulinda familia zao kwa kuwa hakuna kiongozi wa nchi anataka kuona anapoteza nguvu kazi yake hivyo, Rais Dk. Samia anajua thamani ya Watanzania.
"Iwapo nitabaini yupo mwananchi anahujumu vyandarua hivyo kwa kufugia kuku atalipa faini kwa kutozwa vyandarua vingine 10.
Kwa upande wa wananchi wa Nzega akiwemo Richard Sendela mkazi wa Utemi Nzega Mjini amesema vyandarua hivyo ni muhimu hivyo, wanaishukuru Serikali kwa kuwafikia wale wenye hali ya chini ambao hawakuwa na uwezo wa kununua vyandarua vya famili nzima kwa kaya.
“Natumia vyandarua hivi na nimeoa tangu mwaka 1970 nina mke mmoja tumezaa watoto tisa na nina wajukuu 30 na nguvu bado ninazo hayo ni maneno ya uongo vijana wetu wale vizuri,”alisema.
Wakati huo huo Kaimu Meneja wa Bohari ya Dawa(MSD ) Mkoa wa Tabora Adonizedeck Tefurukwa amewahakikishia wananchi wa Nzega wote walio katika mpango wa kupewa vyandarua hivyo baada ya kujiandikisha katika kaya zao watapata kwani vipo vya kutosha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...