Na Said Mwishehe, Michuzi TV
MANISPAA ya Temeke mkoani Dar es Salaam yenye jumla ya watu 1,364,674 imewahimiza wananchi na wakazi wake kuendelea kulipa fedha kupitia kodi na tozo mbalimbali za manispaa kwa hiyari na kwa wakati.
Imesema kwa kufanya hivyo Manispaa itaweza kufikia lengo kwani katika mwaka wa fedha 2023/2024 kiasi cha Sh.24,331,338,000 kimepangwa kutumika kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali huku kiasi kilichopangwa kukusanywa kikiwa ni Sh.47,707,210,000.
Akizungumza wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na mipango ya utekelezaji kwa mwaka 2023/2024 ndani ya manispaa hiyo Meya wa Manispaa ya Temeke Abdallah Mtinika amesema manispaa hiyo inajivunia muamko mkubwa wa wananchi katika kulipa kodi na tozo.
Mtinika amesema Manispaa ya Temeke imekuwa na mipango mbalimbali ya kuendelea kupeleka maendeleo kwa wananchi hivyo ili kufanikisha mipango hiyo iko haja kwa wananchi kulipa kodi hizo ili kupata fedha za ndani zitakazosaidia kufanikisha utekelezaji wa miradi iliyokusudiwa.
“Uongozi unawahimiza wananchi wa Temeke kuendelea kulipa kodi na tozo mbalimbali za manispaa na hatimaye kufanikiwa kutekeleza miradi ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa ambayo kimsingi miradi hiyo ni mali ya wananchi.
“Hata hivyo nitume nafasi hii kuwapongeza wananchi na wakazi wa Temeke kwa muamko mkubwa walionao katika kulipa kodi na tozo za manispaa.Kupitia wananchi wetu katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 tumefikia malengo ya kukusanya zaidi ya Sh.bilioni 43 kwa mwaka uliopita.
“Kwa kweli lazima tupongeze muamko wa wananchi na muamko huu nitoe pongezi kwa viongozi mbalimbali , wenyeviti wa serikali ya mtaa, viongozi wa taasisi kama katika masoko , viongozi wa taasisi za umma mfano hospitali , viongozi wa stendi na wakuu wa vitendo mbalimbali kwani wametusaidia kufikia malengo yetu,”amesema Mtinika.
Aidha amesema muamko huo umetengenezwa pia na madiwani wa kata zote za Manispaa ya Temeke huku akieleza yeye kama Meya amekuwa akisisitiza kwmba ajenda ya ukusanyaji mapato inakuwa ajenda ya kudumu.
Akielezea zaidi kuhusu Temeke amesema kuwa wanahimiza ukusanyaji mapato kwani wanatambua takwimu zilizopo watoto zaidi ya 100 wanazaliwa kila siku ndani ya manispaa hiyo na katika wiki moja zaidi ya watoto 700 wanazaliwa.
“Kwetu sisi sio tatizo bali ni fursa kwani kuwa na idadi kubwa ya watu ni fursa kibiashara, kimapato, fursa kwa rasilimali watu na uwekezaji kwasababu ni nguvu kazi na hakika tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuimarishia miundombinu mbalimbali.
“Kama mnavyoona leo wananchi wenzetu wa Mbagala wanayo barabara ya mwendokasi kwa hiyo kuongezeka kwa watu kunakwenda sambamba na ukuaji wa shughuli za maendeleo , pia tumefungua masoko mbalimbali ambayo tumeendelea kuyatengeneza .
“Kwa hiyo idadi kubwa ya watu Temeke kwetu tunaitumia kama fursa lakini nasi kutokana na hayo tumejipanga kuendana na idadi hiyo.Tunajua ardhi haiongezeki isipokuwa watu wanaongezeka kwa hiyo ukitazama hata mipango yetu utaona inapangwa kulinagana na ongezeko la watu wetu.”
Meya Mtinika akielezea utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka 2022/2023 amesema Temeke ilipanga kukusanya fedha zaidi ya Sh.bilioni 43.4 na kufanikiwa kukusanya zaidi ya Sh.43.10 sawa na asilimia 101 ya lengo walililokuwa wameliweka.
Amesema katika makusanyo hayo Sh.23,120,860,604 zilitengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi , kiasi kilichotumika ni Sh.19,954,259,867.00 na kiasi cha Sh.3,166,600,738.00 kimevuka mwaka(bakaa).
Kuhusu kiasi cha fedha kilichovuka mwaka(bakaa) Mtimika amesema kitatumika katika kutekeleza masual mbalimbali yakiwemo ya kujenga shule za sekondari mkoa, ukamilishaji bweni shule ya sekondari Kibasila , ukarabati wa masoko.
Pia kitatumika katika malipo ya fidia ya wazabuni, ukamilishaji vyumba vya madarasa Shule ya Msingi Upendo na Mmzinga, ukamilishaji vituo vya afya Mkondogwa , Kilakala na Goroka.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...