Na Karama Kenyunko Michuzi TV
SERIKALI ya Tanzania na Norway kupitia Shirika lake la NORAD zimesaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wenye thamani ya Sh bilioni tisa kwa ajili ya kuwezesha kufanyika kwa tafiti zitakazosaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kipindi cha miaka mitano.
Makubaliano hayo yameshuhudiwa na
Waziri wa Nchi , Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, Balozi wa Norway nchini, Tonne Tines na Balozi wa Sweden nchini, Charlotta Macias.
Makubaliano hayo yamefanyika baina ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Watu kutoka Balozi za Norway na Sweden Lisa Sivertsen, na kushuhudiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk Selemani Jafo akiwa na Balozi wa Norway nchini Tonne Tines na Balozi wa Sweden Charlotta.
Akizungumza baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo jijini Dar es Salaam, Waziri Jafo ameipongeza COSTECH kwa jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya utafiti huo .
"Dunia inakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi kama mnavyoona barafu inayeyuka, ukame usiotabirika, mvua za mashaka yote ni athari ya mabadiliko ya tabia nchi. Serikali ya Tanzania imepata pesa kupitia wenzetu wa Norway na Sweden kwa ajili ya utafiti wa mabadiliko ya tabianchi hapa nchini," amesema.
Ameeleza kuwa Tanzania ilijiwekea malengo ya kupambana na gesi hatarishi ili kupambana na mabadiliko hayo kwani wamekusudia mpaka 2030 watapunguza kati ya asilimia 30 hadi asilimi 35 ya gesi hatarishi.
Waziri Jafo amesema kusainiwa kwa makubaliano hayo ni muendelezo wa utekelezaji wa makubaliano ya awali ya Mwezi Septemba mwaka 2023 serikali ya Tanzania ilisaini mkataba na Serikali ua Norway kwa ajili kuimaisha shughuli mbalimbali za uchumi nchini yakiwemo masuala ya ushirikiano wa kupambana na mabadiliko hayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Costech, Dkt Amos Nungu amesema kuwa ufadhili huo utawahusu watafiti wote nchini ili kusaidia kupatikana kwa majibu ya namna bora ya kuikabili hali hiyo.
''Tumesaini makubaliano na Noroway wanatoa ufadhili wa shilingi bilioni tisa kwa miaka mitano kwenye mfuko COSTECH unaofahamika kama MKUSATE kwa ajili ya kufadhili Tafiti zinazohusiana na mabadiliko ya Tabia ya nchi" amesema Nungu
Amesema kuwa tume hiyo ndio inayoratibu tafiti za kisayansi na kwamba kupitia mfuko huo watafiti wote watafadhiliwa.
"Kupitia mfuko huu tutatoa fedha za ufadhili kwa watafiti wote wale wanaotoka kwenye taasisi na umma na wale watafiti wanaotoka kwenye taasisi binafsi," amesema Dk Nungu.
Amesema kuwa anatarajia watafiti wataunda timu itakayotatua changamoto kwenye jamii kwa vile mabadiriko ya tabia ya nchi ndiyo yanayosababisha ukame njaa, wanyama na binadamu wanaathirika kutokana na mabadiliko hayo .
"Kila miaka mitano tutakuwa tunatoa fedha kwa timu ya wataalamu waliokusanyika pamoja na kuja na pendekezo litakaloweza kutatua changamoto za tabianchi .
Naye Balozi wa Norway Tinnes amesema ufadhili huo ni sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa Kwa ajili ya kukubaliana na kupunguza suala zima la mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema mradi huo unahusisha tafiti zinazoweza kutoa elimu kuhusu tabia nchi ambazo zitawasiaida watanzania kuweza kujua kwa kina kuhusu mabadiliko ya tabia nchi athari na namna ya kukabiliana nayo.
Balozi wa Sweden, Macias amesema mradi utaongeza uwezo wa watanzania katika tafiti na kuimarisha taasisi kuhusu tabia nchi na kwamba wako tayari kushiriki.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Watu kutoka Balozi za Norway na Sweden Lisa Sivertsen, (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia, Dkt. Amos Nungu, wakifurahi baada ya kumaliza kutia saini makubaliano ya kufanya tafiti itakayosaidia kupunguza athari za manadiliko ya Tabia Nchi. Katika makubaliano hayo Norway imetoa Sh. Bilioni 9 kwa Costech kwa ajili ya utafiti wa Tabianchi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Suleimani Jafo akizungumza kabla ya serikali kupitia COSTECH na Shirika la NORAD la nchini Norway kusaini mkataba wa makubaliano kwa ajili ya tafiti za tabia nchi wenye ufadhili wa Sh. Bilioni tisa.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...