Na Mwandishi Wetu

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuchukua dhima na dhamana ya kumuenzi Bibi Titi Mohamed kwa vitendo.

Kinana amesema uamuzi wa Rais Dkt. Samia wa kuenzi siku ya kumbukumbu kwa ajili ya Bibi Titi, mwanamke shujaa katika harakati za kupigania uhuru wa nchi, ni ishara ya kutambua mchango mkubwa alioutoa mwana mama huyo kwa taifa.

Makamu Mwenyekiti Kinana ameyasema hayo Novemba 30, 2023 katika wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, katika hafla ambapo Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha miaka miwili na nusu, tukio lililoenda sambamba na na kuanza kwa maadhimisho ya Wiki ya Kumbukumbu ya Bibi Titi Mohamed.

“Nampongeza sana Rais Samia kwa kutambua mchango wa Bibi Titi. Imechukua zaidi ya miaka 60 kwa Tanzania kutambua mchango wake, Rais Samia ametoa fursa hiyo ya kuutambua.

“Naona fahari kuja kushiriki kumbukumbu na maadhimisho ya Bibi Titi Mohamed wa Rufiji. Ni mpigania uhuru wa Tanzania, naamini kabisa ukitaka majina matatu muhimu ya ukombozi wa nchi yetu baada ya Baba wa Taifa na Mzee Rashid Mfaume Kawawa kwa Bara, atakayefuata ni Bibi Titi Mohamed.

“Tunakila sababu ya kujivunia Bibi Titi Mohamed aliyejitolea maisha yake, afya yake, familia yake kwa ajili ya ukombozi wa taifa letu. Hakuwa na elimu, lakini Mwenyezi Mungu alimjalia uwezo, maarifa, busara na dhima ya uongozi, kila aliposema alisikilizwa,” amefafanua Makamu Mwenyekiti Kinana.

Aliongeza kuwa, Bibi Titi kila alipotoa mwongozo alifuatwa na alikuwa ni mkono wa kushoto wa Baba wa Taifa wakati Mzee Rashid Kawawa akiwa mkono wa kulia.

Kutokana na mchango wa mwana mama huyo kwa taifa, Kinana alisema Watanzania wanayo kila sababu ya kuona fahari kwa kuwa na mwanamke shupavu aliyejituma na kujitolea kwa taifa.Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...