SERIKALI imeeleza dhamira yake ya kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi unakwenda sambamba na heshima na ulinzi wa haki za binadamu kwa kila raia.
“Tunataka watu waishi katika usawa na haki, huku tukikuza uchumi wa taifa,”
Hayo amesema Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Katiba na Sheria Zanzibar, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kuandaa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu na Biashara, Mzee Ali Haji, akizungumza na waandishi wa habari leo, Juni 4, 2025 jijini Dar es Salaam, mara baada ya kikao cha Kamati iliyopitia na kuidhinisha rasimu ya mwisho ya Mpango Kazi kutoka kwa Timu ya Wataalamu kwa lengo la kumalizia uandaaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu na Biashara.
Timu hiyo ya Wataalamu imekamilisha mchakato wa kuandaa Mpango kazi huo mara baada ya kuunganisha mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati ya Kitaifa kwenye kikao chake cha 4 pamoja na mapendekezo kutoka kwa wadau mbalimbali zikiwemo wizara, taasisi za serikali, na Asasi za Kiraia
Akizungumza kuhusu mpango huo, Mzee Ali Haji alisema: “Leo, tumekutana hapa kama Kamati ya Kitaifa kwa ajili ya kuhitimisha mchakato wa kuandaa mpango huu muhimu. Mpango huu umeangazia maeneo mbalimbali ya kiuchumi, ikiwemo utalii na uchumi wa buluu, viwanda, biashara, na madini, kwa lengo la kuhakikisha kuwa utekelezaji wa shughuli katika sekta hizo unazingatia haki za binadamu ambazo ni msingi wa mafanikio tunayoyatarajia kama taifa.”
Ameeleza kuwa mpango huo unalenga kuhakikisha haki za binadamu na sheria za kazi zinazingatiwa ipasavyo katika maeneo yote ya maendeleo kuanzia utalii, uchumi wa buluu, viwanda, biashara, madini, hadi uwekezaji.
“Tunaangalia changamoto zilizopo katika maeneo kama vile biashara, uchimbaji wa madini, na masuala ya ardhi kwa kuzingatia namna haki za binadamu zinavyoweza kulindwa,” amefafanua.
Ameongeza kuwa mpango kazi huo umechambua kwa kina masuala ya haki katika sekta ya viwanda, ikiwa ni pamoja na tekelezaji wa sheria za kazi (kama muda wa kazi), Mazingira salama ya kufanyia kazi na Kukomesha unyanyasaji kazini.
Aidha, amehoji iwapo mishahara inayotolewa katika sekta mbalimbali inalingana na kazi inayofanywa na kama inazingatia viwango vya kimataifa. Katika kila sekta, mpango huo umechunguza utekelezaji wa sheria za kitaifa na kimataifa ili kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na kila mdau anatekeleza wajibu wake kwa haki na usawa.
Mzee Ali Haji pia ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa juhudi zao kubwa katika kuhakikisha haki za binadamu zinazingatiwa katika mipango yote ya maendeleo ya taifa.
Mpango kazi huu ni rasimu inayotarajiwa kukabidhiwa rasmi serikalini kabla ya kuanza kwa mwaka wa fedha 2025/2026. Matarajio ya serikali ni kwamba, kupitia utekelezaji wake, kila mwananchi atakuwa na uhakika wa kufanya kazi katika mazingira ya haki, usawa, na ulinzi wa sheria za kitaifa na kimataifa.
.jpeg)
Matukio mbalimbali katika kikao cha Kamati iliyopitia na kuidhinisha rasimu ya mwisho ya Mpango Kazi kutoka kwa Timu ya Wataalamu kwa lengo la kumalizia uandaaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu na Biashara. Kikao hicho kimefanyika jijini Dar es Salaam leo Juni 4, 2025.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...