Tunduru-Ruvuma.
Changamoto ya huduma ya majisafi na salama kwa wakazi wa mji wa Tunduru Mkoani Ruvuma,inakwenda kumalizika baada ya Serikali kutoa zaidi ya Sh.bilioni 3,400,814,000 ili kuongeza upatikanaji na kuboresha huduma ya maji katika Mji huo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Tunduru Mjini(TUWASA) Mhandisi Cuthbert Kiwia wakati akizungumza na Wanahabari Ofisini kwake mjini Tunduru.
Amesema,kupitia fedha hizo watekeleza mradi mkubwa utakaozalisha lita milioni 8,214,000 wakati kwa sasa mahitaji ya maji kwa wananchi wa Mji wa Tunduru ni lita milioni 6.8, hivyo mradi huo utawezesha wananchi kupata huduma ya maji kwa asilimia 100 kwani mtandao wa mabomba nao utaongeza kwa kilometa 98.6.
Katika mji wa Tunduru maeneo mengi hayakuwa na mtandao wa maji ya bomba,lakini kupitia mradi huo huduma ya maji itaongezeka kwa kuwa watapeleka mtandao kwenye maeneo mengi ya mji wa Tunduru kwa ajili ya kusambaza huduma ya maji kilinganisha na sasa ambapo mtandao wa mabomba katika mji huo ni kilometa 3.3.
“Kupitia mradi huu tunajenga tenki kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 1 kwa kuwa matenki yaliyopo yana ujazo wa lita laki 6 tu huku mahitaji wananchi ni ujazo wa lita milioni 1.6,tenki linajengwa katika eneo la juu kuliko eneo lolote katika mji wa Tunduru na ujenzi wake umefikia asilimia 20”alisema Kiwia.
Aidha amebainisha kuwa, katika kipindi cha miaka minne 2021 - 2025 huduma ya maji imeongezeka kutoka asilimia 46 hadi kufikia asilimia 78 na hali hiyo imetokana na jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyehakikisha wananchi wanapata huduma ya maji.
Kiwia ameeleza kuwa,chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan Tuwasa imetekeleza miradi mbalimbali ya maji yenye gharama ya Sh.bilioni 4.8 ikiwemo mradi wa kufunga umeme jua(Solar Power) uliosaidia kuongeza upatikanaji wa maji kutokana na changamoto ya umeme iliyopo katika mji wa Tunduru.
“katika jitihada zetu kuhakikisha huduma ya majisafi inapatikana kwa wananchi tumechimba visima viwili vyenye uwezo wa kuzalishaji maji lita milioni 2,280,000 kwa siku,hivyo karibu asilimia 61 ya maji yanayopatikana katika mji wa Tunduru yanatoka katika visima hivi”alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka hiyo Jonathan Haule,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha na kuongeza upatikanaji wa majisafi na salama kwa wananchi wa mji wa Tunduru.
Amesema mradi utatekelezwa kwa muda wa miezi mitano na lengo la mradi huo ni kwa ajili ya kusambaza huduma ya majisafi na salama kwa wananchi ili waweze kunufaika na uwekezaji mkubwa wa Serikali yao ya awamu ya sita chini ya kauli mbiu ya kumtua mama ndoo kichwani.
Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Mchangani Ali Shaibu,ameipongeza Serikali kwa kuanza kutekeleza mradi huo unaokwenda kumaliza kabisa changamoto ya maji kwa wananchi wa mtaa huo na Mji wa Tunduru kwa ujumla.
Mkazi wa Mchangani Sofia Adam amesema, katika mtaa wa Mchangani changamoto kubwa iliyopo kwa muda mrefu ni huduma ya majisafi na salama na kupelekea kutumia maji ya visima vya asili na wengine kutumia maji ya visima walivyochimba wenyewe ambavyo maji yake hayafai kwa matumizi ya binadamu.
“wakati mwingine maji tunapata lakini kero iliyopo maji hayo yanatolewa kwa mgao,hivyo mradi huu utakuwa suluhisho la kudumu kwa kuwa utamaliza changamoto tuliyonayo”alisema Adam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...