Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Yohane Kihaga akikabidhi moja ya baiskeli kwa Mhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Yohane Kihaga akikabidhi moja ya baiskeli kwa Mhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii.

Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (Mabalozi wa Fistula) katika picha ya pamoja na baiskeli zao mpya.

Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (Mabalozi wa Fistula) katika picha ya pamoja na baiskeli zao mpya.


***
Geita; 4 Julai 2025: Amref Health Africa – Tanzania, kupitia ufadhili kutoka Buffalo Bicycles Tanzania, imekabidhi jumla ya baiskeli 250 zenye thamani ya Tshs. 132,500,000/= (Milioni Mia moja thelathini na mbili na laki tano) kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (Mabalozi wa Fistula) Mkoani Geita ili kuongeza uwezo wa kuwafikia na kuwaibua wanawake waliopata au walio hatarini kupata fistula ya uzazi, hasa katika maeneo ya vijijini.


Makabidhiano hayo yamefanyika katika hafla rasmi iliyoandaliwa kwa ushirikiano na Uongozi wa Mkoa wa Geita, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha huduma za afya ya uzazi na kutokomeza kabisa fistula ya uzazi, mojawapo ya changamoto kubwa za afya ya wanawake nchini.


Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mgeni Rasmi, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Yohane Kihaga amesema:
“Baiskeli hizi si tu zitarahisisha kazi ya Mabalozi wa Fistula, bali pia zitachochea mapinduzi ya kweli katika upatikanaji wa huduma za afya ya Mama na Mtotohususani waliopo maeneo ya vijijini. Tunawapongeza Amref Tanzania na Buffalo Bicycles Tanzania kwa mchango huu mkubwa katika jitihada za kuboresha afya ya Mama na Mtoto.”


Kwa upande wake, Gaspery Misungwi Meneja wa Mradi wa Fistula kutoka Amref Tanzania alisisitiza umuhimu wa uwekezaji katika jamii kupitia wahudumu wa afya ngazi ya jamii yaani mabalozi:


“Kupitia msaada huu kutoka Buffalo Bicycles Tanzania, tunawapatia mabalozi wetu uwezo wa kufika mbali zaidi – kuokoa maisha, kurejesha utu na kupunguza unyanyapaa kwa wahanga wa fistula ya Uzazi. Huu ni uwekezaji wa moja kwa moja katika afya na haki za wanawake na watoto.”


Kwa upande wake, Rehema Richard, Meneja Tathmini na Ufuatiliaji wa Shirika la Buffalo Bicycles Tanzania amesema baiskeli hizo ni mchango kutoka Shirika la Buffalo Bicycles Tanzania, likiwa ni sehemu ya ushirikiano wa kimkakati unaolenga kuwawezesha wahudumu wa afya kuwafikia wananchi kwa haraka na kwa ufanisi.


“Tunaamini kwamba baiskeli bora ni daraja muhimu kwa mtoa huduma kufikia walengwa kwa wakati. Kwa kushirikiana na Amref, tunawezesha mabadiliko ya kweli katika maisha ya watu kwa kusaidia upatikanaji wa huduma muhimu, hasa katika maeneo ya vijijini,” amesema.




Baiskeli hizo zitawawezesha Mabalozi wa Fistula kufikia maeneo ya mbali kwa wakati na urahisi zaidi, pamoja na kuwafuatilia wanawake waliopata au walioko hatarini kupata fistula.

Pia zitaimarisha uwezo wao wa kufanya rufaa za haraka kwa wajawazito na wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura, hatua ambayo itaokoa maisha na kuboresha ustawi wa jamii.

Aidha, mabalozi hao wataweza kutoa elimu ya afya ya uzazi, fistula na haki za wanawake katika maeneo ya vijijini. Vilevile, watakuwa na nafasi ya kukusanya taarifa muhimu za afya zinazosaidia katika kufanya maamuzi ya kisera kwa usahihi na ufanisi zaidi.
Amref Tanzania inatekeleza mradi huu kama sehemu ya harakati zake za zaidi ya miaka 20 katika mapambano dhidi ya fistula, kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania na wadau wa kimataifa. Lengo ni kuhakikisha huduma za afya ya uzazi zinapatikana kwa wakati, kwa usawa na kwa staha bila mwanamke yeyote kuachwa nyuma.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Yohane Kihaga akizungumza wakati wa makabidhiano ya baiskeli 250 kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii Mkoani Geita.

Gaspery Misungwi, Meneja wa Mradi wa Fistula kutoka Amref Tanzania akizungumza wakati wa makabidhiano ya baiskeli 250 kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii Mkoani Geita.


Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (Mabalozi wa Fistula) katika picha ya pamoja na basikeli zao mpya.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...