Na Daudi Nyingo, Njombe

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede, ameongoza zoezi la utambuzi na uchanjaji wa mifugo mkoani Njombe, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo kwa Mifugo iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa mkoani Simiyu hivi karibuni.

Akizungumza na wananchi na wataalamu wa mifugo Julai 4, 2025, Dkt. Mhede alisema kuwa Serikali kupitia wizara yake imejipanga kuhakikisha mifugo yote nchini inapatiwa chanjo dhidi ya magonjwa hatarishi na kuhakikisha kuwa kila chanjo iliyokusudiwa imewasili na kusambazwa kulingana na mahitaji.

"Tunachanja mifugo kwa maana ya ng’ombe dhidi ya homa ya mapafu na tunachanja kuku dhidi ya magonjwa ya kideri, mafua na ndui vilevile tumefika na kuthibitisha kuwa chanjo zote zimefika, na wataalamu waliopatiwa mafunzo wapo kazini kwa ari kubwa wakizingatia miongozo ya wizara "

“Serikali imechukua jukumu kubwa la kugharamia chanjo hizo pamoja na kuwezesha wataalamu wa mifugo, jambo ambalo ninyi wafugaji mmelipongeza. Nimefurahi mmeonesha ari kubwa na kupongeza hatua ya serikali kwa kuwashika mkono kwa zaidi ya asilimia 50 kupitia uwezeshaji wa kitaalamu na chanjo,” alisema Dkt. Mhede.

Dkt. Mhede, aliongeza kuwa kupitia zoezi hilo Serikali imepata nafasi kujifunza changamoto za moja kwa moja kutoka kwa wafugaji, zikiwemo masuala ya soko la bidhaa za mifugo. Ameahidi kukaa na pamoja na wadau kuona namna ya kuongeza thamani ya mazao kwa kujenga viwanda vya kusindika maziwa na kuimarisha upatikanaji wa masoko ndani na nje ya Njombe.

Nae Afisa Mifugo wa Mkoa wa Njombe, Bw. Nicolas Buji, akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, alisema kuwa katika zoezi la uchanjaji wa mifugo, serikali imechangia kwa kiasi kikubwa ili kuhakikisha kila mfugaji anapata huduma hiyo kwa gharama nafuu.

"Kwa chanjo ya homa ya mapafu kwa ng’ombe, mfugaji anachangia shilingi 500 tu kwa kila ng’ombe, huku serikali ikichangia kiasi kikubwa zaidi ili kumwezesha mfugaji kudhibiti ugonjwa huu hatari. Kwa upande wa kuku, serikali imegharamia chanjo kwa asilimia mia moja na hivyo chanjo inatolewa bure kabisa kwa wafugaji. Mkoa wa Njombe unalenga kuchanja ng’ombe takribani 240,000 na kuku zaidi ya milioni 1.3 katika halmashauri zote za mkoa, kwa lengo la kuhakikisha mifugo yote inapata kinga dhidi ya magonjwa hatarishi." alisema Bw. Buji.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Bw. Mathias Mbafu, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuleta kampeni ya kitaifa ya uchanjaji wa mifugo, akisema ni mkombozi mkubwa kwa wafugaji wa maeneo ya vijijini kwani Wafugaji walikuwa wanapata changamoto kubwa kutokana na mifugo kuathirika kiafya kwa kukosa chanjo, na walikuwa wakitumia gharama kubwa kutibu badala ya kujikinga. Halmashauri imejipanga, wataalamu wako tayari na ameahidi kutoa ushirikiano kuhakikisha mifugo yote inachanjwa.

Naye Meneja wa Shamba la Mifugo Kitulo lililopo Wilaya ni Makete, Bw. Joseph Mlelwa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wadau wote wanaohusika mpango huu. Ametoa rai kwa wafugaji kote nchini kuitikia wito wa kuwachanja ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku wao, kwani serikali imeshatoa ruzuku ya kugharamia uchanjaji na utambuzi wa mifugo

Mkoa wa Njombe unakadiriwa kuwa na ng’ombe wapatao 240,000 na kuku zaidi ya milioni 1.3. chanjo zote zinazohitajika zimefika kulingana na idadi hiyo, kwa lengo la kuimarisha afya ya mifugo na kupatikana kwa mazao bora kwa walaji.

Kampeni ya uchanjaji na utambuzi inaendelea nchi nzima kwa kipindi cha miezi mitatu ili kufikia adhima ya serikali ya kuwa na mifugo yenye afya bora, tija na yenye thamani ya kiuchumi kwa wafugaji na watumiaji wa mazao ya mifugo.



Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede (kulia) akishuhudia zoezi la uwekaji wa heleni kwa ng’ombe alipotembelea wafugaji wa mkoa wa Njombe Julai 04, 2025, ikiwa ni muendelezo wa zoezi la uhamasishaji utoaji chanjo na utambuzi wa mifugo iliyofanyika katika Wilaya ya Makete, mkoani Njombe.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede (kulia) akiongoza zoezi la uchanjaji wa mifugo (kuku) alipotembelea wafugaji wa mkoa wa Njombe Julai 04, 2025, ikiwa ni muendelezo wa zoezi la uhamasishaji utoaji chanjo na utambuzi wa mifugo iliyofanyika katika Wilaya ya Makete, mkoani Njombe.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede (kulia) akikabidhi vitendea kazi vitakavyotumika kwenye zoezi la uchanjaji na utambuzi wa mifugo kwa Afisa Mifugo wa Mkoa wa Njombe, Bw. Nicolas Buji (wa pili kulia) alipotembelea wafugaji wa mkoa huo Julai 04, 2025, ikiwa ni muendelezo wa zoezi la uhamasishaji utoaji chanjo na utambuzi wa mifugo iliyofanyika katika Mtaa wa Lunyani, Wilaya ya Njombe mkoani Njombe.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede akisikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wafugaji Halmashauri ya Mji wa Njombe kutoka kwa baadhi ya wafugaji waliojitokeza kuchanja na kutambua mifugo yao alipotembelea wafugaji wa Halmashauri hiyo Julai 04, 2025 ikiwa ni muendelezo wa zoezi la uhamasishaji utoaji chanjo na utambuzi wa mifugo iliyofanyika katika Mtaa wa Lunyani, Wilaya ya Njombe mkoani Njombe.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede akipata maelezo kuhusiana na uendeshwaji wa zoezi la uchanjaji na utambuzi wa mifugo kutoka kwa Daktari wa Mifugo Halmashauri ya Mji wa Njombe Dkt. Godphrey Kongo alipotembelea wafugaji wa Halmashauri hiyo Julai 04, 2025 ikiwa ni muendelezo wa zoezi la uhamasishaji utoaji chanjo na utambuzi wa mifugo iliyofanyika katika Mtaa wa Lunyani, Wilaya ya Njombe mkoani Njombe.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...