NA WILLIUM PAUL, SIHA. 

WANAFUNZI wa kata ya Mitimirefu wilayani Siha mkoani Kilimanjaro waliokuwa wakitembea umbali wa kilomita 15, kufuata shule ya sekondari Namwai wanaenda kuondokana na changamoto hiyo baada ya serikali kutoa fedha milioni 584.2 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya.
Mwenge wa Uhuru 2025 ulifika kujionea ujenzi wa shule hiyo na kuweka jiwe la msingi, ambapo wazazi walieleza jinsi watoto wao walivyokuwa wakikatisha masomo yao kutokana na umbali huo. 


Amina Mollel alisema kuwa, wanafunzi wa kike wamekuwa wakikumbana na vishawishi kutoka kwa vijana wasio wazalendo hali ambayo imepelekea kukatishwa masomo yao kwa kubeba ujauzito na wakati mwingine kutoroshwa. 
"Ujenzi wa hii shule utakapokamilika utakuwa mkombozi kwa watoto wetu hasa wa kike maana wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi wanapokuwa wanaenda au kurudi kutoka shule hali ambayo wakati mwingine imekuwa ikichangia kukatisha masomo yao" Alisema Amina. 


Naye Leonard Lukumai alisema kuwa, kukamilika kwa shule hiyo kutachangia kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi kwani wamekuwa wakikumbana na changamoto ya kutembea umbali mrefu hali ambayo imekuwa ikipelekea wafike shule wakiwa wamechoka. 


Akisoma taarifa za ujenzi wa Kiongozi wa mbio za Mwenge, Ismail Ali Ussi, Kaimu Mkuu wa shule hiyo, Said Ngagama alisema kuwa Shule ya Sekondari Namwai ilipokea kiasi cha fedha cha shilingi 584,280,029.00 kupitia Mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ikiwa ni kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari katika Kata ya Mitimirefu.


Alisema kuwa, lengo la Mradi huu ni kusogeza huduma ya Elimu kwa wanafunzi ambao wanatembea 
umbali wa zaidi ya kilometa 15 kila siku kwenda Shule ya sekondari ya Namwai na kurudi nyumbani kwao (katika Kata ya Mitimirefu).

Aliongeza kuwa mradi huo umehusisha ujenzi  wa vyumba 8 vya madarasa na Ofisi 2, Jengo 1 la Utawala, maabara 3 za masomo ya Sayansi ambayo ni Kemia, Biolojia na Fizikia, chumba 1 cha Tehama, chumba 1 cha Maktaba, matundu 8 ya vyoo vya kawaida pamoja na matundu 2 ya vyoo kwa 
wanafunzi wenye mahitaji maalumu. 

Alisema kuwa pia utahusisha tenki 
la maji (tank raiser) na kichomea taka (Incinerator) ambapo pia mradi huo unagharamia pia ununuzi 
wa samani kwa ajili ya Wanafunzi na Walimu. 

"Shule hii itakapo kamilika inauwezo wa kupokea wanafunzi 320 wa kidato cha Kwanza hadi kidato cha Nne na katika utekelezaji wa Mradi huu wananchi wapatao 63 wameweza kupata ajira za muda kupitia Mradi huu ambao umefika asilimia 62" Alisema 


Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge 2025, Ismail Ali Ussi alisema kuwa, serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya elimu kwa kuhakikisha wanafunzi hawatembei umbali mrefu kufuata shule. 

Ussi alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuyatunza mejango hayo ambayo serikali imewekeza fedha nyingi ili yaweze kudumu kwa muda mrefu na lengo la serikali liweze kutimia.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...