Dar es Salaam, Novemba 21, 2025 — Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Profesa Palamagamba Kabudi, amewataka waandishi wa vitabu nchini kuwa wabunifu katika kazi zao ili kuongeza hamasa ya usomaji na kuimarisha umoja wa Watanzania.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 32 ya Kimataifa ya Vitabu Tanzania, Waziri Kabudi amesema ubunifu katika uandishi ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi, kulinda amani na kuhifadhi utamaduni wa Taifa.

“Tasnia ya uandishi wa vitabu ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuhifadhi utamaduni. Uandishi unaozingatia ubunifu huongeza hamasa kwa wasomaji pamoja na kujenga uzalendo, uwezo wa kutafakari, kujiamini na kutoendeshwa na mkumbo,” alisema Prof. Kabudi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania, Dkt. Mboni Ruzegea, amesema serikali imeanza kuimarisha maktaba za jamii na maktaba mtandao ili kukuza usomaji wa vitabu, sambamba na kuanza ununuzi wa vitabu kutoka kwa waandishi wa ndani.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wachapishaji wa Vitabu Tanzania (PATA), Ndg. Hermes Damian, alisema sekta ya uandishi wa vitabu inakabiliwa na changamoto za kisera na kimiongozo. Aidha, Mjumbe wa Bodi kutoka Chama cha Wachapishaji wa Kenya, Ndg. Musyoki Muli, alipendekeza kuanzishwa kwa maonesho ya kikanda ya uandishi wa vitabu Afrika Mashariki ili kukuza sekta hiyo kwa ngazi ya kimataifa.

Maonesho ya mwaka huu yatafanyika kwa siku sita kuanzia Novemba 21 hadi 26, yakibeba kaulimbiu: “Vitabu ni hifadhi ya maarifa na utamaduni”. Washiriki wake ni waandishi wa vitabu, wachapishaji, wasomaji na wadau wa sekta ya elimu na utamaduni kutoka ndani na nje ya nchi.


















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...