Na Mwandishi Wetu
Morogoro. Benki ya Absa imetoa msaada wa mahitaji muhimu kwa watoto yatima wanaolelewa katika kituo cha Raya Islamic Orphanage Centre kilichopo kijiji cha Lugono wilayani Mvomero, mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya mchango wa benki hiyo na wafanyakazi wake katika kuunga mkono juhudi za malezi na kuboresha ustawi wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo kwa walezi na watoto kituoni hapo jana, Meneja wa Tawi la Absa Mkoa wa Morogoro, Godfrey Chilewa, alisema hatua hiyo ni muendelezo wa benki hiyo katika kurudisha fadhila kwa jamii inayowazunguka. Alisema kituo hicho ni miongoni mwa maeneo wanayoyafikia kwa lengo la kupunguza changamoto za malezi zinazowakabili watoto yatima na wenye mazingira magumu.

Chilewa alisema benki hiyo inatambua kazi kubwa inayofanywa na vituo vya kuhudumia watoto yatima nchini, na kwamba changamoto wanazopitia zinahitaji nguvu ya pamoja kutoka kwa watu binafsi, taasisi na makampuni ili kuhakikisha watoto hao wanapata huduma bora na makuzi salama.

“Watoto yatima wana uhitaji sawa wa malezi kama watoto wengine wanaokua katika familia zao, watoto hawa nao wana story za maisha yao wangependa zitimie, sisi Absa tunasema ‘Stori yako ina thamani’, Stori za maisha ya watoto hawa zina thamani kwetu na tunaamini misaada kama hii inakwenda kuchangia kukamilika kwa stori zao.

“Mara nyingi watoto wanaolelewa kwenye vituo wanakosa baadhi ya mahitaji ya msingi kutokana na uwezo mdogo wa vituo hivyo. Hivyo, ni jukumu letu kama jamii kusaidia kile tunachokipata ili watoto hawa wakue kama wengine,” alisema Chilewa.

Akiendelea kueleza, alisema jamii ina wajibu wa kusaidia kujenga kizazi chenye maarifa, uwezo wa kujitegemea na dira sahihi, huku akisisitiza kuwa watoto yatima mara nyingi hukosa huduma muhimu kama chakula, mavazi, elimu na afya. Aliongeza kuwa ndoto ya Absa ni kuona changamoto hizo zinapungua kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali akiongeza kuwa hii inaenda sambamba na lengo la benki hiyo la ‘Kuiwezesha Afrika na Tanzania ya Kesho, Pamoja, hatua moja baada ya nyingi’.

Saidi Hamis (27), mmoja wa vijana waliokulia kituoni hapo, alisema kituo hicho kina jumla ya watoto 113, ambapo wavulana ni 66 na wasichana 47. Alieleza kuwa kituo kilianzishwa mwaka 2013 eneo la Mindu kabla ya kuhamia Lugono, na kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa uzio wa kuzunguka makazi yao.

“Changamoto kubwa ni kukosa uzio, jambo ambalo linatuweka katika hatari ya kuvamiwa na wanyama wakali, ikiwemo tembo wanaotoroka Hifadhi ya Taifa ya Mikumi. Tunaiomba jamii kutusaidia kufanikisha ujenzi wa uzio ili watoto wawe salama,” alisema Saidi.

Kwa upande wake, Karomelo Kizilahabi (17), mmoja wa watoto wanaolelewa kituoni, alisema msaada walioupokea utawasaidia kwa kiasi kikubwa, hasa cherehani nne walizokabidhiwa ambazo zitawawezesha kujifunza ufundi wa kushona nguo.

“Cherehani hizi zitatusaidia kupata ujuzi wa kushona nguo na kutujengea uwezo wa kujitegemea baadaye. Tunawashukuru kwa kutukumbuka na tunawaombea muendelee kuwa na moyo huu,” alisema Karomelo.
Meneja wa Tawi la Benki ya Absa Mkoa wa Morogoro, Bw. Godfrey Chilewa (katikati) na Ofisa wa kitengo cha fedha wa benki hiyo, Bi. Aiva Mussa, wakikabidhi kichwa cha chereheni kwa Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Raya Islamic Orphanage Centre Lugono, Bw. Ramadhani Msombeli, katika hafla ambayo benki hiyo ilikabidhi msaada  wa mahitaji mengine muhimu yakiwemo vyakula, sabuni na vinywaji, kituoni hapo,  mkoani Morogoro, jana. 
Meneja wa Tawi la Benki ya Absa Mkoa wa Morogoro, Bw. Godfrey Chilewa (Katikati) na Ofisa wa kitengo cha mauzo wa benki hiyo, Bi. Grace Ndile wakikabidhi mfuko wa unga kwa Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Raya Islamic Orphanage Centre Lugono, Bw. Ramadhani Msombeli katika hafla ambayo benki hiyo ilikabidhi msaada wa mahitaji muhimu vikiwemo vyakula, sabuni, vinywaji na cherehani, kituoni hapo, mkoani Morogoro, jana.
Meneja wa Tawi la Benki ya Absa Mkoa wa Morogoro, Bw. Godfrey Chilewa (Katikati) na Meneja Masoko wa benki hiyo, Bw. Shauri Masengwa wakiwakabidhi vinywaji watoto, Karomelo Kizilahabi na Jamali Abdallah, katika hafla ambayo benki hiyo ilikabidhi msaada wa mahitaji muhimu vikiwemo  vyakula, sabuni na cherehani, kwa kituo cha Raya Islamic Orphanage Centre Lugono wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, jana.
Meneja wa Tawi la Benki ya Absa Mkoa wa Morogoro, Bw. Godfrey Chilewa kushoto  na baadhi wafanyakazi wenzake wa tawi hilo, wakiwa na baadhi ya watoto yatima wa Kituo cha Raya Islamic Orphanage Centre kilichopo Lugono wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, baada ya kukabidhi msaada wa mahitaji muhimu vikiwemo vyakula, sabuni, vinywaji na cherehani, kituoni hapo jana.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...