Na Mwandishi Wetu

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE),kimesema kimeendelea kufanya vizuri kitaaluma ambapo utafiti uliofanyika mwaka jana ulikiweka kwenye nafsi ya nane kati ya vyuo 47 vya elimu ya juu.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Edda Lwoga, wakati wa kongamano la kitaaluma lililofanyika chuoni hapo.

Alisema chuo hicho kikongwe kimetimiza miaka 60 ya kubobea kwenye kufundisha biashara, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA na kwa muda wote wa uhai wake kimemudu kuzalisha idadi kubwa ya wataalamu wa kada mbalimbali.

Alisema kwa sasa chuo hicho kina kampasi nne za Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Mbeya na mwakani kinatarajia kujenga kampasi yake nyingine mkoani Kilimanjaro kutimiza ahadi iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa kampeni zake.

Alisema katika kudhihirisha ubora wake utafiti uliofanyika mwaka jana ulionyesha chuo hicho kushika nafasi ya nane kati ya vyuo 47 vya elimu ya juu nchini na kwamba mafanikio hayo yamewezeshwa kwa mshikamano na walimu na wanafunzi.

Alisema 2018 kampasi zote nne zilikuwa na jumla ya wanafunzi 7,000 lakini kwa sasa wako 23,111 na program 68 katika Nyanja za uchumi, biashar, uongozi TEHAMA na vipimo.

Alisema chuo kimeendelea kufanya vizuri kwa ubora wa elimu na kimeendelea kuhakikisha program zake zote zinafanyika kwa vitendo na mwaka 2018 walianzisha program ya atamizi za biashara.

“Tulianzisha program atamizi ili wanafunzi wenye bunifu zao za biashara wazilete tuziatamie ziweze kukua na kuwa biashara kubwa, wewe mgeni rasmi ni shahidi wakati unapita kwenye mabanda yetu umeona vijana waliotengeneza mfumo wa umwagiliaji kidijitali na mfumo wa ukodishaji magari,” alisema

Aidha, alisema tangu kuanza kwa program hiyo wanafunzi 770 wameshaleta bunifu zao na wameweza kuzilea na wako katika hatua mbalimbali na wanafunzi walioleta kwa Dar es Salaam pekee ni 361.

Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Ushindani (FCC), Khadija Ngasongwa aliwapongeza wanafunzi wa chuo hicho kwa ubunifu wa program mbalimbali na kuutaka uongozi wa chuo kwenda kusajili ubunifu huo.

“Elimu mnayoipata hapa msiichukulie poa kabisa ni elimu ambayo inaenda kuwapa maisha huko mtaani, siyo lazima mkimbilie katika ajira mnaweza kutumia ujuzi mliopata kujiajiri na mkafanikiwa,” alisema

“Msikae kinyonge, mmepata elimu ambayo inaweza kuwafikisha kwenye safari ya kujikwamua kiuchumi, “ alisema



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...