Na Mwandishi Wetu
WADAU  kutoka sekta mbalimbali za umma na binafsi wamekubaliana juu ya mbinu ya ushirikishwaji wa jamii ili kuharakisha matumizi ya teknolojia za nishati safi ya kupikia nchini Tanzania wakati wa warsha ya kitaifa ya majadiliano iliyofanyika Dodoma.

Warsha hiyo iliwaleta pamoja wawakilishi kutoka taasisi za serikali, taasisi za kifedha, watoa huduma za nishati kutoka sekta binafsi, taasisi za viwango, mashirika ya kiraia, taasisi za utafiti, vyombo vya habari, makundi ya wanawake na vijana, pamoja na washirika wa maendeleo, kwa lengo la kujadili na kuafikiana kuhusu hatua za kipaumbele zitakazosaidia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa Tanzania (2024–2034) wenye lengo la kuona walau asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka huo.

Majadiliano yalilenga kuimarisha uratibu, kuongeza uelewa wa watumiaji, kushughulikia vikwazo vya mila na kitamaduni, pamoja na kusaidia suluhisho za masoko na ufadhili ili kupunguza utegemezi wa nishati ya jadi ikiwemo matumizi ya kuni. Washiriki walisisitiza kuwa nishati safi ya kupikia ni muhimu katika kuboresha afya ya umma, kulinda mazingira, na kuwawezesha wanawake.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mhandisi Anitha Ringia kutoka Wizara ya Nishati alisema kuwa serikali inaipa kipaumbele nishati safi ya kupikia kama sehemu ya ajenda pana ya nishati na maendeleo, akibainisha kuwa utekelezaji wenye mafanikio unahitaji ushirikiano kati ya wizara, sekta binafsi, taasisi za kifedha na jamii.

Michango iliyotolewa na wadau wakati wa warsha hiyo itatumika kuandaa Mkakati wa Ushirikishwaji wa Wadau na Uhamasishaji, unaolenga kufafanua majukumu, kuimarisha uratibu, na kuongoza namna ya kushirikisha wadau wote katika mfumo wa nishati safi ya kupikia.

Akitoa maoni kuhusu umuhimu wa mashauriano hayo, Fidelis Luteganya, Afisa Uwekezaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Maendeleo (UNCDF), alisema ushirikishwaji huo wa wadau ni muhimu katika kuhakikisha kuwa afua za nishati safi ya kupikia zinazingatia hali halisi ya masoko na mahitaji ya kaya.

“Ili suluhisho za nishati safi ya kupikia ziweze kusambaa kwa kiwango kikubwa, tunahitaji zaidi ya teknolojia—tunahitaji uratibu imara, uwe wa masoko na ufadhili kwa ajili ya kaya na biashara kwa pamoja. Mashauriano haya yaliwasaidia wadau kuafikiana juu ya njia za vitendo zinazoweza kufungua uwekezaji na kuharakisha matumizi,” alisema.

Mashauriano hayo yalikuwa sehemu ya juhudi zinazoendelea za kampeni ya uhamasishaji chini ya Mpango wa CookFund wa UNCDF, unaotekelezwa nchini Tanzania kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya kwa ushirikiano na Kengo Limited. Ushirikishwaji huo ulitoa fursa ya kuhakikisha kuwa mbinu zinazopendekezwa ni za vitendo, jumuishi, na zinazingatia hali mbalimbali za kaya za Watanzania.

Washiriki walisisitiza umuhimu wa uhakiki wa ubora, mawasiliano yaliyo wazi kuhusu teknolojia za nishati safi ya kupikia, pamoja na mifumo ya ufadhili inayofanya teknolojia za kisasa za kupikia zipatikane kwa kaya zenye viwango tofauti vya kipato.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji kutoka Kampuni ya ushauri na usimamizi wa biashara (Kengo Limited), Bi. Sarah Majengo amesema lengo la kukutanisha wadau wa masuala ya Nishati safi ya kupikia ni kutambua wadau muhimu katika utekelezaji, majukumu yao, namna ya kuwafikia pamoja na kuendelea kukusanya maoni mbalimbali ambayo yatasaidia kutekeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia sambamba na kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Wananchi.

“Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni agenda mahususi ambayo imechukua nafasi kubwa katika Sera, Mipango na Mikakati ya Serikali, umuhimu wa agenda hii unasukumwa na ongezeko la uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi” amesema Majengo.

Ameeleza kuwa, ushirikishwaji wa wadau utasaidia ujumbe wa nishati safi ya kupikia kufika kwa watu sahihi, kwa kuzingatia jinsia, majukumu ya kijamii pia utumiaji wa lugha ambayo inaeleweka kwa kila mwananchi.

Wizara ya Nishati inatarajiwa kuchapisha Mkakati wa Ushirikishwaji wa Wadau na Uhamasishaji kama sehemu ya juhudi zake zinazoendelea za kuunga mkono jitihada hizi kuelekea nishati ya kupikia iliyo salama, nafuu, na endelevu kote nchini.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...