WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Watanzania wanataka kuiona nchi yao ikifikisha lengo la uchumi wa kati wa dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050 na watakaofanikisha jambo hilo ni sekta binafsi ikiwemo wenye wabunifu kutoka kwenye kampuni changa.

“Mtakumbuka kuwa Julai, mwaka huu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua DIRA 2050. Dira hii si ya Serikali peke yake bali ni kielelezo cha matarajio ya Watanzania ambao wanataka nchi yao ifikie uchumi wa kati wa dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050. Injini ya kuendesha nchi kuelekea maono haya ni sekta binafsi zikiwemo kampuni changa zinazoanzishwa,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Desemba 03, 2025) wakati akifunga maadhimisho ya Wiki ya Kampuni Changa za Teknolojia (start-ups) kwenye ukumbi wa PSSSF, Makumbusho, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kazi ya kufikisha lengo siyo ndogo na inahitaji mabadiliko ya kiutendaji na kimtazamo. “Hatuwezi kufikia uchumi wa dola trilioni moja kwa kuendelea kuuza bidhaa ghafi au kufanya mabadiliko kidogo tu. Inatutaka tuwe na mbinu bunifu zenye tija: tuwe na njia mipya za kufanya mambo, tuanzishe makampuni mapya, tuwe na bidhaa mpya na teknolojia mpya zinazoweza kukua mara 10 badala ya asilimia 10.”

“Inahitaji tuje na ubunifu wa Kitanzania utakaovutia mataifa na kuzalisha masoko ya nje. Inawezekana kabisa, twendeni tuunganishe nguvu,” amesisitiza.

Amesema vijana waliochukua hatua ya kuanzisha kampuni changa wao ndiyo wenye hatma ya Tanzania na kwambo njia hiyo ndiyo sahihi ya kutenda kwa njia mbadala. “Nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na changamoto ya vijana kutojiamini. Lakini wapo wengi ambao wametoa ajira kwa vijana wenzao. Na hii ndiyo njia sahihi ya kufanya mambo kwa njia mbadala kama ambavyo wenzeyu wamefanya.”

Amewataka Watanzania waiheshimu sekta binafsi kama wanavyoiheshimu sekta ya umma kwa kuanza kubadilisha mtazamo wao ikiwemo nidhamu ya utendaji kazi. “Kwa mazingira ya sasa, hakuna nchi imeweza kujenga uchumi mkubwa bila kuishirikisha sekta binafsi. Hiki mnachokifanya ndiyo injini ya kukuza uchumi,” amesema.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa maadhimisho hayo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Anjela Kairuki alisema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kampuni changa ambapo hadi sasa kampuni changa za Kitanzania zinakadiriwa kufikia 1,041 na kuzalisha ajira zaidi ya 140,000.

Alisema hadi kufikia mwaka 2024, kampuni hizo zilikuwa zimeingiza mapato ya dola za marekani milioni 96.4 na kwamba hadi kufikia sasa zimekwishafikisha mapato ya dola za Marekani milioni 300.

Alisema kampuni nyingi zinazochipukia zimejielekeza kwenye matumizi ya teknolojia za huduma za kifedha, kilimo, afya, elimu na kwamba bado wanatarajia kuwa na bunifu nyingi za kidijitali.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...