
Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
SERIKALI imeweka mkazo kwa vijana wa Tanzania kuachana na uchumi wa uchuuzi na usambazaji wa bidhaa kutoka nje, na badala yake kuelekeza nguvu zao katika uzalishaji na utengenezaji wa bidhaa ndani ya nchi ili kujenga uchumi imara na wenye tija. Wito huo umetolewa na Waziri wa Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Mnanauka, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu dira na dhamira ya Serikali katika kuwawezesha vijana kiuchumi.
Waziri Mnanauka amesema maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona vijana wanakuwa wamiliki wa uchumi, wazalishaji na watengenezaji wa ajira, badala ya kuwa wachuuzi na wasambazaji wa bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi. Alisisitiza kuwa mwelekeo huo ndio msingi wa kaulimbiu ya wizara isemayo “Vijana Tuyajenge Tanzania Yetu.”
Alieleza kuwa kwa mara ya kwanza nchini, Rais ameunda wizara maalum inayoshughulikia maendeleo ya vijana, ikiwa chini ya Ofisi ya Rais, hatua inayodhihirisha dhamira ya dhati ya Serikali kuhakikisha vijana wanasikilizwa, wanafikiwa walipo na wanashirikishwa kikamilifu katika kujenga mustakabali wa taifa.
Kwa mujibu wa Waziri, Serikali imetambua kuwa vijana ndio nguvu kazi kubwa ya taifa, ambapo kwa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35 ni zaidi ya milioni 20.6 kati ya Watanzania milioni 60.
Hali hiyo, amesema, inaitaka Serikali kuwekeza kwa makusudi katika mifumo itakayowainua vijana kiuchumi kupitia uzalishaji, viwanda vidogo na kati pamoja na biashara zenye kuongeza thamani.
Akifafanua hatua mahsusi, Mnanauka amesema Serikali imeimarisha utekelezaji wa sheria za manunuzi ya umma zinazotaka taasisi za Serikali kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa makundi maalum yakiwemo makampuni ya vijana. Kupitia mpango huo, zaidi ya shilingi bilioni 10.8 tayari zimeelekezwa kwenye makampuni madogo ya vijana kati ya mwaka 2021 hadi 2025, hatua inayolenga kukuza kampuni hizo na si kuwapa vijana fedha ndogondogo zisizo na tija ya muda mrefu.
Vilevile, Serikali imeanzisha mkakati wa Youth Investment Program na kuandaa mpango wa kuanzisha Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Vijana (Youth Special Economic Zones) yatakayowezesha vijana kupata mitaji, mitambo, miundombinu ya uhakika kama umeme na maji, pamoja na huduma zote za kiserikali katika eneo moja. Lengo ni kuwa na kampuni za vijana zipatazo laki moja ndani ya miaka mitano, huku angalau kampuni 20,000 zikiwepo ndani ya maeneo hayo maalum ya uzalishaji.
“Dhamira yetu ni kutoka kwenye uchumi wa uchuuzi na kuingia kwenye uchumi wa uzalishaji na utengenezaji. Tunataka vijana wazalishe, wachakate na waongeze thamani rasilimali zetu, ili wasiwe tu watafuta ajira bali pia wawe watengenezaji wa ajira,” amesema Mnanauka.
Katika kukabiliana na changamoto ya mitaji, Waziri amesema Serikali inaweka mkazo kwenye mifumo ya dhamana za mikopo (credit guarantee schemes), ufadhili wa mitambo (asset financing), pamoja na madirisha maalum ya uwekezaji kwa vijana katika benki.
Aidha, amesisitiza kuwa kila mpango wa uwezeshaji vijana utaambatana na malezi, usimamizi na ushauri wa kibiashara (mentorship) ili kuhakikisha miradi inakuwa endelevu.
Serikali pia inaendelea kuimarisha mafunzo kazini, urasimishaji wa ujuzi kwa vijana waliopata stadi nje ya mifumo rasmi ya elimu, pamoja na kukuza ajira katika sekta za kilimo, uvuvi, madini, viwanda na uchumi wa kidijitali.
Kwa upande wa utekelezaji, Mnanauka amesema wizara inaongozwa na falsafa tatu kuu: kasi katika utoaji huduma, viongozi kufikika kwa vijana, na matumizi ya teknolojia, ikiwemo uanzishaji wa jukwaa la kidijitali la huduma jumuishi kwa vijana ili kuwaunganisha na fursa za ajira, mitaji na masoko.
Amehitimisha kwa kutoa wito kwa vijana wa Tanzania kuwa wazalendo, wachapa kazi na wabunifu, wakisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili vijana wawe mhimili wa uchumi wa taifa.
“Vijana sio tatizo, vijana ni suluhisho.
Tunataka kuona simulizi inabadilika, kutoka vijana kuwa changamoto, hadi vijana kuwa injini ya maendeleo ya Taifa,” amesema.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...