Na Mwandishi Wetu – WMTH, Dar es Salaam

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), leo tarehe 02 Desemba 2025, amefanya ziara ya kikazi katika ofisi za Tume ya TEHAMA (ICT Commission) jijini Dar es Salaam, ambako amesisitiza umuhimu wa kuendeleza fursa za TEHAMA na kuboresha taaluma kwa wataalamu wa sekta hiyo.

Akizungumza na menejimenti ya Tume, Mhe. Kairuki ameelekeza kuanzishwa kwa mfumo wa kupima kiwango cha maendeleo ya TEHAMA kwa mwaka (ICT Ranking) utakaoonesha mafanikio, changamoto na maeneo yanayohitaji maboresho. Amesema mfumo huo utaleta ushindani chanya baina ya taasisi na kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa programu mbalimbali za TEHAMA.

Aidha, Waziri Kairuki ameitaka Tume ya TEHAMA kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara, Taasisi za Serikali na sekta binafsi ili kuongeza nguvu ya pamoja katika kuendeleza teknolojia nchini. Pia ameagiza kuanzishwa kwa majukwaa ya uwekezaji katika TEHAMA yatakayowakutanisha wadau, wabunifu, wawekezaji na vijana wanaojikita katika ubunifu.

Katika hatua nyingine, amewapongeza watendaji wa Tume kwa kuanzisha utamaduni wa kutambua na kuzawadia ubunifu, akisema hatua hiyo inaleta ari na ushindani wenye tija kwa vijana na wataalamu chipukizi wanaoshiriki katika programu za TEHAMA.

Waziri Kairuki amesisitiza pia kuongeza kasi ya ufunguaji wa ICT Hubs katika vyuo, shule za kata na maeneo ya jamii, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma za broadband, hususan vijijini, ili kuhakikisha wananchi wote wananufaika na uchumi wa kidijitali.

Awali, akiwasilisha taarifa kwa niaba ya Menejimenti ya Tume ya TEHAMA, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Moses Mwasaga, alimkaribisha Waziri na kumweleza mafanikio yaliyopatikana, ikiwemo maandalizi ya mapendekezo ya Kituo cha Ubunifu cha Afrika (Africa AI Centre Proposal) na hatua za awali za kuandaa mfumo mkubwa wa lugha ya Kiswahili (Swahili Large Language Models) ili kukuza matumizi ya teknolojia za kizazi kipya zenye msingi wa akili bandia.

Mhe. Kairuki amewataka watendaji wa Tume kufanya kazi kwa ubunifu, kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango, na kuhakikisha Watanzania—hasa vijana—wanapata nafasi pana ya kutumia teknolojia katika kuchochea uchumi wa taifa.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...