NA DENIS MLOWE, IRINGA
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mheshimiwa Rahma Kisuo, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo na uendelezaji ujuzi, wakati akifunga mafunzo ya wakulima na wasindikaji wadogo sambamba na kuzindua Muongozo wa Kitaifa wa Uratibu wa Mafunzo ya Kuongeza Ujuzi kwa mwaka 2026.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Royal Palm, Manispaa ya Iringa, Mheshimiwa Kisuo alisema uzinduzi wa muongozo huo ni hatua mahsusi katika kuhakikisha nguvu kazi ya Taifa inapewa ujuzi unaoendana na mahitaji ya sasa ya soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia.
"Ninachukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri, wenye maono na dhamira thabiti ya kuendeleza sekta ya kilimo na kuboresha huduma kwa wananchi. Mageuzi haya tunayoyaona leo ni matokeo ya uongozi wake makini," alisema Kisuo.
Mheshimiwa Kisuo alisema licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima na wasindikaji wadogo, wameonyesha dhamira ya dhati ya kujifunza na kuongeza ujuzi, hatua inayoongeza tija na ushindani katika soko.
Akiwapongeza washiriki, alisema:
"Nawapongeza wakulima na wasindikaji wote. Mmekuja kwa wingi takribani washiriki 250 kutoka Mkoa wa Iringa na wengine 315 kutoka mikoa ya Mbeya, Singida na Dodoma. Hii ni ishara ya ari ya kujifunza na kuboresha uzalishaji."
Alisema mafunzo hayo yamelenga kupunguza pengo la ujuzi nchini, ili kuwezesha nguvu kazi kushindana katika soko la ajira na kukidhi mahitaji ya sekta zinazokua kwa kasi.
Akifafanua kuhusu dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mheshimiwa Kisuo alisema sekta za kimkakati kama kilimo, bado zinahitaji nguvu kazi yenye ujuzi wa kati na wa juu ili kuongeza mchango wake katika pato la taifa.
"Lengo letu kufikia mwaka 2050, ni kuwa na nguvu kazi yenye ujuzi unaoakisi mahitaji ya nchi za uchumi wa kati ujuzi wa chini usizidi asilimia 54 na ujuzi wa kati usipungue asilimia 34," alisema.
Serikali, alisema, imeandaa mpango mahsusi wa kuhakikisha nguvu kazi inapewa ujuzi wa ziada na stadi za kazi ili kuongeza ufanisi na uzalishaji na mageuzi Makubwa Katika Sekta ya Kilimo Chini ya Serikali ya Awamu ya Sita
Mheshimiwa Kisuo alisisitiza kuwa mafanikio yanayoonekana leo yanatokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na serikali katika kilimo, ikiwa ni pamoja na Kuongeza bajeti ya sekta, kuimarisha upatikanaji wa mbolea za ruzuku, kuboresha tafiti za mbegu bora. kupeleka teknolojia za kisasa kwa wakulima, Kukuza matumizi ya kilimo hai na kuboresha uhifadhi wa mazao
"Tumeona kwa kiasi kikubwa nchi ikijitosheleza kwa chakula kwa zaidi ya asilimia 120. Haya ni mafanikio makubwa ambayo kila Mtanzania anapaswa kujivunia," aliongeza.
Akihitimisha, Naibu Waziri aliwataka wahitimu wa mafunzo hayo kuwa mabalozi wa ujuzi na mabadiliko katika maeneo yao.
"Twendeni tukatumie ujuzi huu kuongeza tija, kuongeza kipato, kuboresha afya ya jamii, na kuchangia uchumi wa taifa. Ujuzi wenu ni msingi wa maendeleo ya kilimo na viwanda vyetu," alisema.
Awali meneja wa Umoja wa Ushirika wa Wakulima Mkoa wa Iringa (Iringa Farmers Cooperative Union – IFCU), Tumaini Lupola, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa namna inavyowezesha sekta ya kilimo kupitia ruzuku za pembejeo, mafunzo na ujenzi wa uwezo kwa wakulima, hatua inayowezesha ongezeko la uzalishaji na kipato kwa wakulima mkoani humo.
Lupola alisema chama hicho kimekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza wajibu wake kwa wanachama na wakulima, hususan katika usambazaji wa pembejeo kama vile mbolea ya ruzuku, mbegu bora na viuatilifu.
“Malengo yetu ni kuongeza tija na ubora wa mazao, kuongeza kipato kwa wakulima na kuimarisha usalama wa chakula nchini,” alisema Lupola.
Lupola aliongeza kuwa IFCU imekuwa ikifanya kazi ya kuwawezesha wanachama, viongozi wa vyama vya ushirika na wakulima kupitia mafunzo mbalimbali ya capacity building, ili kuimarisha uendeshaji wa vyama na kutatua changamoto zinazowakabili wakulima.
Aidha, alisema chama hicho kinaendelea kuchukua hatua za kutatua changamoto za masoko, ili kuhakikisha wakulima wanapata bei shindani na kunufaika zaidi na jasho lao.
Ujenzi wa miundombinu na viwanda vya kuongeza thamani
Katika jitihada za kuboresha kilimo, IFCU imeendelea kujenga maghala na miundombinu ya uhifadhi wa mazao, pamoja na kutekeleza miradi ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani, ili kuhakikisha mazao yanaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu na kufikia viwango vinavyohitajika sokoni.
Akizungumzia kilimo cha mazao lishe, Lupola alisema chama hicho, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kama Harvest Plus na We Effect, kimewezesha wakulima kuzalisha mazao lishe kama mahindi lishe, maharage lishe na viazi lishe, ambayo yana virutubisho muhimu kama vitamini A, protini, madini ya chuma na zinki.
Alibainisha kuwa ushirikiano na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) umechangia upatikanaji wa mbegu bora za mazao hayo, ambazo zimesambazwa kwa wakulima kwa ajili ya uzalishaji na elimu kwa jamii.
Mafunzo ya kuongeza ujuzi yazidi kuleta matokeo
Lupola aliipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana kwa kutoa mafunzo ya ukaushaji, usindikaji na uhifadhi wa mazao, ambayo yameongeza ujuzi wa wakulima na wasindikaji, na kuchagiza juhudi za IFCU katika kuongeza thamani ya mazao.
Iringa ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa zao la nyanya, ambapo takribani asilimia 30 ya vyama vya ushirika huzalisha zao hilo. Hata hivyo, Lupola alitaja changamoto zinazolikabili zao hilo kuwa ni pamoja na ukosefu wa vyumba baridi (cold rooms), umbali wa masoko, na uhaba wa elimu sahihi ya uzalishaji na usindikaji.
IFCU imetoa wito kwa serikali kuongeza wigo wa mafunzo ili wakulima wengi zaidi wapate maarifa ya uzalishaji, usindikaji na uhifadhi wa nyanya, mchicha na mazao mengine.
Wakulima wanufaika wa mafunzo wathibitisha mafanikio
Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, Noela Mapunda, alisema elimu waliyoipata ni muhimu kwa kuongeza tija na kukabiliana na changamoto za lishe na masoko.
“Tumejifunza kuhusu mimea yenye virutubisho vingi kama mtisha nafaka, ambayo ina vitamini A, B, K na madini kama zinc, potassium, calcium na phosphorus,” alisema Noela.
Alisema mafunzo hayo yatawawezesha wakulima kuongeza kipato, kuboresha afya ya jamii na kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo.
IFCU yaendelea kuhimiza matumizi ya pembejeo za ruzuku
Naye Naibu Katibu mkuu shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Cde Rehema Ludanga aliishukuru pia Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua thamani ya Mtanzania na kuendeleza juhudi za kuboresha mifumo ya uongezaji ujuzi ili kuchochea maendeleo ya uchumi na uzalishaji.
“Muongozo huu wa kitaifa ni nguzo muhimu katika kuendesha mafunzo ya kuongeza ujuzi, yakilenga kukuza maendeleo ya rasilimali watu na uchumi wa Taifa letu,” alisema.
.jpg)
.jpg)
.jpg)



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...