Dar es Salaam —

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Leonard Akwilapo, amelielekeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuimarisha utafiti na ubunifu katika sekta ya ujenzi ili kubuni mbinu na teknolojia zitakazowezesha Watanzania wengi zaidi kupata nyumba bora, salama na zenye gharama nafuu.

Waziri Akwilapo alitoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya kikazi NHC, akisisitiza kuwa utafiti wa kina ni msingi wa kupunguza gharama za ujenzi bila kuathiri ubora, sambamba na kuendana na mahitaji halisi ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Alieleza kuwa kupitia tafiti za kisayansi na matumizi ya teknolojia bunifu, NHC itaweza kubuni aina za nyumba na mifumo ya ujenzi itakayozingatia uwezo wa kiuchumi wa wananchi, hali ya hewa, upatikanaji wa vifaa vya ujenzi pamoja na mitindo ya maisha ya jamii husika.

“Utafiti ni njia sahihi ya kupata suluhisho la kudumu. Tukifanya utafiti wa kutosha, tutajenga nyumba zenye ubora, gharama nafuu na zitakazowafikia Watanzania wengi zaidi,” alisema Waziri Akwilapo.

Aidha, Waziri amesema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za NHC katika utafiti na maendeleo (R&D), ikiwemo ushirikiano na taasisi za elimu ya juu, wataalam wa ujenzi na wadau wa sekta binafsi, ili kuongeza tija na ubunifu katika miradi ya makazi.

Katika ziara hiyo, Waziri Akwilapo pia ameipongeza menejimenti na wafanyakazi wa NHC kwa mchango wao mkubwa katika utekelezaji wa agenda ya Serikali ya kuwapatia Watanzania makazi bora, salama na yenye hadhi, akibainisha kuwa mafanikio ya Shirika yanaakisi weledi, uwajibikaji na uzalendo wa watumishi wake.

“NHC ni taasisi muhimu katika kutafsiri maono ya Serikali ya makazi bora kuwa uhalisia. Mafanikio mnayoyapata ni ushahidi wa kujituma na ufanisi wa wafanyakazi wake,” aliongeza.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya, amewataka wafanyakazi wa NHC kuwa mfano bora wa kuishi katika nyumba bora za makazi, ikiwemo kujenga au kumiliki nyumba zao binafsi, ili kuonesha kwa vitendo kile wanachokisimamia kitaaluma na kujimudu kiuchumi.

Naibu Waziri Mmuya alisisitiza kuwa wafanyakazi wa NHC wanapaswa kuwa kielelezo cha mafanikio ya sera na mikakati ya makazi bora, huku wakitekeleza majukumu yao kwa ufanisi, nidhamu na heshima.

Kwa msisitizo wa kipekee na wa kuhamasisha, Mmuya alisema hatategemea kuona wafanyakazi wa NHC wakiwa na tabia ya “wapiga debe” wa madaladala, wakihamasisha wengine kupanda magari ya umma huku wao wenyewe wakiachwa vituoni, badala ya kuwa mfano wa kujimudu na kupanga maisha yao kwa hadhi inayolingana na dhamana waliyonayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah alimhakikishia Waziri kuwa Shirika litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kuzingatia sera na miongozo ya Serikali na kuhakikisha miradi yote inawanufaisha wananchi na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.

Ziara hiyo imeacha taswira chanya ya ushirikiano thabiti kati ya Serikali na NHC, ikidhihirisha azma ya pamoja ya kujenga Tanzania yenye makazi bora, mipango madhubuti ya miji na maisha yenye heshima kwa wananchi wote.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...