Benki ya Exim Tanzania imezindua rasmi Tawi lake jipya Paje, Zanzibar, ikiwa ni hatua ya kimkakati inayolenga kusogeza huduma za kifedha karibu na wateja, kuimarisha mchango wa sekta ya fedha katika uchumi wa Zanzibar, na kuunga mkono ukuaji wa sekta ya utalii, ambayo ni nguzo muhimu ya maendeleo ya visiwa hivyo.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na Mgeni Rasmi, Dkt. Juma Malik Akili, Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, wawakilishi wa taasisi za kifedha, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu, amesema kufunguliwa kwa tawi la Paje ni sehemu ya mkakati wa benki kuimarisha ujumuishi wa kifedha na kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

“Uzinduzi wa tawi hili haupanui tu wigo wa huduma zetu, bali unathibitisha dhamira yetu ya kukuza uwezeshaji wa kiuchumi na kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wananchi walipo,” amesema Matundu.

Katika kipindi cha miaka 28 tangu kuanzishwa kwake, Benki ya Exim imeendelea kukua na kujijengea nafasi miongoni mwa taasisi zinazoongoza za kifedha nchini. Benki hiyo ni ya kwanza kutoka Tanzania kupeleka huduma zake nje ya nchi, ikiwa na uwepo katika Comoros, Djibouti, Uganda pamoja na ofisi wakilishi Ethiopia.

Ndani ya mwaka uliopita, benki ilifungua matawi mapya Kahama na Ubungo, huku mwaka huu ikianza na Paje kabla ya kuelekea Geita kwa uzinduzi mwingine. Upanuzi huo unalenga kuwafikishia wananchi huduma bora za kifedha, ikiwemo ufadhili wa biashara na suluhisho za kidijitali.

Paje ni moja ya maeneo yanayokua kwa kasi kiuchumi Zanzibar, likichochewa na ukuaji wa sekta ya utalii ambayo ni mhimili wa uchumi wa buluu. Kupitia tawi hili, Benki ya Exim inalenga kuhudumia mahitaji ya kifedha ya wawekezaji wa utalii, wavuvi, wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Benki ya Exim imeendelea kuimarisha suluhisho zake za kifedha, ikiwemo huduma ya Supply Chain Finance, inayowawezesha wafanyabiashara katika mnyororo wa thamani kupata ufadhili wa muda mfupi kwa haraka na kwa urahisi, bila masharti ya dhamana ya ziada. Huduma hii inalenga kurahisisha malipo, kuboresha mtiririko wa fedha na kuongeza tija katika biashara.

Akizungumza katika hafla hiyo, mgeni rasmi, Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Juma Malik Akil, alisema:

“Kufunguliwa kwa Tawi la Exim Benki hapa Paje ni hatua muhimu inayosaidia kukuza uchumi wa Zanzibar, hususan katika maeneo ya utalii. Uwepo wa huduma za kifedha zilizo karibu na wawekezaji na wafanyabiashara unachochea ukuaji wa biashara, ajira na mapato ya wananchi. Serikali inaendelea kuhimiza ushirikiano wa karibu na sekta ya fedha katika safari ya maendeleo endelevu.”

Mbali na huduma za kifedha, kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (Exim Cares), Benki ya Exim imeendelea kuchangia katika sekta za afya, elimu, mazingira na uwezeshaji wa jamii, ikiwemo kampeni za uchangiaji damu kwa kushirikiana na Huduma ya Taifa ya Damu Salama (NBTS), kuchangia vifaa tiba katika hospitali mbalimbali, kushiriki miradi ya upandaji miti na uhifadhi wa mazingira, pamoja na kuchangia ukarabati wa huduma za afya kwa watoto navijana wenye changamoto ya afya ya akili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Vilevile, Benki inatarajia kutoa madawati kwa Skuli ya Paje pamoja na samani za ofisi kwa Kituo kipya cha Polisi cha Paje hatua inayodhihirisha dhamira yake ya kuwekeza katika misingi imara ya maendeleo kwa kutambua kuwa elimu bora na usalama wa jamii ni nguzo muhimu za maendeleo endelevu na mazingira wezeshi ya biashara.

Aidha, Benki ya Exim imeonesha mshikamano na kuunga mkono jamii, kwa kuandaa hafla ya futari ya Ramadhani tarehe 20 Februari 2026, ikiwashirikisha wateja wao, wadau, na viongozi wa jamii. Tukio hili limedhihirisha dhamira ya Benki hiyo ya kushirikiana na jamii, kujali, mshikamano, unyenyekevu, na kuimarisha mshikamano kwa kijamii sambamba na kutoa huduma zake za kifedha visiwani Zanzibar.

Uzinduzi wa Tawi hilo unaimarisha nafasi ya Benki ya Exim kama mshirika wa maendeleo wa serikali, sekta ya binafsi, na jamii, huku ikiendelea kutoa huduma za kifedha zinazochangia ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi wa Zanzibar hususan katika sekta ya utalii na Tanzania kwa ujumla.
Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dkt. Juma Malik Akili (Wa pili kulia) pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Jafari Matundu (Wa pili kushoto)wakikata utepe kama ishara ya kufungua kwa tawi jipya la Benki hiyo Paje, linalolenga Kusogeza huduma kwa wananchi na wafanya Biashara wa eneo hilo na kusaidia katika kukuza Utalii na uchumi wa buluu wa Zanzibar. Tukio hilo limeshudiwa na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Bunafsi wa Benki ya Exim TanzaniaAndrew Lyimo (Kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja, Mhe. Othman Ali Maulid (kulia).Hafla hiyo imefanyika tarehe 21 Februari 2026 Visiwani Paje Zanzibar.













Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...