*π Bilioni 6.8 zaongeza matumaini ya nishati safi Kisemvule, Pwani*
*π Wananchi wengi zaidi kusambaziwa gesi asilia kwa mkoa wa Pwani na Lindi*
Kisemvule, Pwaniπ
Utekelezaji wa mradi wa kusambaza gesi asili katika eneo la Kisemvule, wilayani Mkuranga mkoani Pwani, umeendelea kuibua matumaini mapya kwa Wananchi wa eneo hilo ambapo zaidi ya shilingi bilioni 6.8 zimewekezwa katika kusambaza gesi asilia katika maeneo yaliyopitiwa na mkuza wa bomba la gesi asilia.
Mradi huo umejengwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kufadhiliwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania watakuwa wanatumia nishati safi ya kupikia.
Akizungumza baada ya kutembelea na kukagua Mradi huo; Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi na Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu, amesema utekelezaji wa Mradi huo unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuboresha maisha ya Wananchi na kulinda mazingira.
Amesema Bodi ya Nishati Vijijini inajivunia kuona mwitikio mkubwa wa Wananchi wanaene kuhamasika kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kutumia gesi asili, ambayo ni salama, nafuu na rafiki kwa mazingira.
“Huu ni Mradi wa kimkakati unaotekeleza maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuona Watanzania wengi wanatumia nishati safi, tunapaswa kulinda miundombinu hii kwa kuwa imegharimu fedha nyingi za Serikali,” amesema Balozi Kingu.
Kwa mujibu wa REA, mradi huo wa mfano ulilenga kuhudumia kaya 2,000 huku hadi sasa kaya 530 zikiwa zimefikiwa na huduma hiyo katika eneo la Kisemvule lenye wakazi zaidi ya 64,000 hali inayotoa fursa ya kupanua zaidi wigo wa huduma hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi, Hassan Saidy amesema taasisi hiyo imeiomba TPDC kufanya tathmini katika maeneo yenye idadi kubwa ya watu ambako bomba la gesi limepita ili kuanzisha miradi ya ubia itakayowezesha wananchi wengi zaidi kuunganishwa na huduma hiyo.
Ametaja baadhi ya maeneo yanayopendekezwa kuwa ni Mkuranga Mjini, Ikwiriri na Kilwa Kivinje, akibainisha kuwa hatua hiyo itaharakisha utekelezaji wa Sera ya Nishati Safi nchini.
Naye Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia za Nishati Mbadala kutoka REA, Mhandisi, Advera Mwijage amesema Bodi ya Nishati Vijijini imeagiza kuongeza kasi ya uunganishwaji wa kaya zaidi ili Mradi huo unufaishe Wananchi wengi zaidi kulingana na mahitaji halisi ya eneo hilo.
Kwa upande wake, Mhandisi, Tumaini Daniel, Meneja Mradi kutoka TPDC amesema Mradi huo umekamilika kwa mafanikio na umeweka msingi mzuri wa upanuzi wa huduma hiyo katika maeneo mengine yenye miundombinu ya bomba la gesi.
Wananchi wa Kisemvule wameanza kunufaika matokeo chanya ya Mradi huo, wakieleza kupungua kwa gharama za matumizi ya nishati na urahisi wa upatikanaji wa gesi asilia kupitia mifumo ya malipo ya simu.
Mradi huo unaendelea kuwa mfano wa utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Nishati Safi ukionesha namna uwekezaji wa kimkakati unavyoweza kubadilisha maisha ya Wanancha ili kulinda mazingira na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika ngazi ya jamii.








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...