📍Ahimiza ulinza wa miundombinu na mapambano dhidi ya ukatili
NA MWANDISHI WETU, MBEYA
MKUU wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomon Itunda, amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa, katika hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Polisi cha Kata ya Igoma, kilichogharimu Shilingi milioni 150.
Hatua hiyo ni mkakati wa serikali kuimarisha ulinzi, usalama, na kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliokwenda sambamba na makabidhiano ya miundombinu hiyo, Mhe. Itunda amesema ujenzi wa kituo hicho ni matokeo ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha mazingira ya kazi ya vyombo vya ulinzi nchini.
Mhe. Itunda amebainisha kuwa uwekezaji huo mkubwa katika sekta ya usalama unalenga kudumisha amani na utulivu, mambo ambayo ni nguzo kuu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi ndani ya Mkoa wa Mbeya na taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa onyo kali kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Alisema serikali haitafanya muhali kwa yeyote atakayebainika kukiuka haki za wengine na amewataka wananchi kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa za uhalifu kwa vyombo vya dola.
Aidha, Mhe. Itunda amewataka wakazi wa Igoma na maeneo jirani kukitunza kituo hicho kipya na kuona miundombinu hiyo kama mali yao, ili iweze kudumu na kutoa huduma kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya polisi na jamii (Polisi Jamii) ndiyo silaha pekee ya kutokomeza uhalifu.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi waandamizi wa Jeshi la Polisi, akiwemo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya (RPC), Benjamin Kuzaga, pamoja na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Mbalizi (OCD), ambao kwa pamoja wameahidi kuongeza ufanisi wa kazi kutokana na kupatikana kwa kituo hicho kipya.


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...