
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (katikati) akikata utepe ishara ya kuzindua helikopta ya kisasa ya Kampuni ya Barrick kwa ajili ya kufanya utafiti wa kijiolojia wa anga - Picha na Kadama Malunde


Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akipata maelezo wakati akizindua helikopta ya kisasa ya Kampuni ya Barrick kwa ajili ya kufanya utafiti wa kijiolojia wa anga

Helikopta ya kisasa ya Kampuni ya Barrick kwa ajili ya kufanya utafiti wa kijiolojia wa anga

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde na viongozi ,mbalimbali wakishuhudia helikopta ya kisasa ya Kampuni ya Barrick ikiruka angani kwa ajili ya kufanya utafiti wa kijiolojia wa anga

Helikopta ya kisasa ya Kampuni ya Barrick ikiwa angani

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akizungumza wakati akizindua helikopta ya kisasa ya Kampuni ya Barrick kwa ajili ya kufanya utafiti wa kijiolojia wa anga
Meneja wa Barrick nchini , Dkt. Melkiory Ngido akizungumza wakati wa hafla hiyo
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita akizungumza wakati wa hafla hiyo.
**
Kampuni ya Barrick ambayo inaendesha shughuli zake kwa ubia na serikali kupitia Twiga Minerals leo imezindua helikopta ya kisasa kwa ajili ya kufanya utafiti wa kijiolojia wa anga wenye kupunguza athari za kimazingira na kuboresha shughuli za utafutaji wa madini nchini.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa utafiti huo wa kutumia helikopta , Wilayani Kahama , Mkoani Shinyanga, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema kwamba hatua hii ni muhimu katika kuimarisha sekta ya madini ya nchini na kufungua milango ya tafiti kwa kutumia nyenzo za kisasa zaidi.
Waziri Mavunde amesema uwekezaji wa teknolojia ya kisasa ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa sera ya madini ya Taifa , inayolenga kuimarisha utafiti wa rasiliamali madini, kuongeza thamani ya sekta ya madini katika uchumi wa taifa, na kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa ufanisi zaidi.

“Moja ya hatua kubwa kwa kampuni ya Barrick nchini kwa kushirikiana na kampuni ya Twiga Minerals ya serikali katika kufanya tafiti zaidi kwa njia ya kisayansi zaidi kwa lengo la kupanua wigo wa maeneo mapya ya utafiti na uwekezaji kwenye sekta ya madini nchini,”ameongeza Mavunde.
Ameongeza kuwa hatua hiyo ni ya kihistoria katika kufanya tafiti kwa njia ya helikopta kwa sababu utafiti wa madini ni sayansi inahitaji uwekezaji mkubwa.
"Kupitia Dira ya Madini 2030: Madini ni Maisha na Utajiri, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuelekeza kuhakikisha tunaongeza eneo la utafiti wa kina wa madini kupitia uwekezaji wa Serikali na Sekta binafsi"
"Tunachokifanya leo hapa ni kiashiria tosha kwamba maono hayo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yanakwenda kufikiwa ipasavyo. Tunaishukuru Kampuni ya Barrick kwa kuamua kuunga mkono juhudi hizi za Serikali kwa vitendo", ameeleza Mhe. Mavunde.
Amefafanua Kampuni ya Barrick imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye tafiti na baada ya uzinduzi wa helikopta utafiti wake utagusa maeneo ya Nzega, Igunga , Msalala na Nyangh’wale katika Mkoa wa Shinyanga.
“Naipongeza Barrick kwa kuendelea kuwekeza kwenye eneo la tafiti kwa sababu dunia ya leo huwezi kukwepa utafiti katika shughuli za utafutaji wa madini ,” amesema Mavunde.

Akiongea katika hafla hiyo, Meneja wa Barrick nchini , Dkt. Melkiory Ngido amesema kwamba ni hatua kubwa kwa kampuni hiyo kwa kushirikiana na serikali katika uzinduzi wa helikopta ya kisasa ya utafiti wa kijiolojia wa anga, itakayosaidia shughuli za utafutaji wa madini kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu.
Ameongeza kwamba kampuni ya Barrick inatarajiwa kufanya tafiti ya kijiolojia wa kutumia teknolojia ya hali ya juu na kisasa zaidi (high-resolution airborne geophysical surveys) ambayo huongeza usahihi wa upatikanaji wa taarifa za miamba iliyo chini ya ardhi, kupunguza athari za kimazingira na kuboresha ufanisi wa shughuli za utafutaji wa madini.
Ngido amesema uzinduzi wa tafiti hiyo ambayo itatumia helikopta , unaakisi dhamira ya kampuni ya Barrick kuendeleza kuwekeza nchini na kutafuta maeneo yatakayofaa kuanzia mgodi mkubwa ili kuleta mchango wa muda mrefu kwa maendeleo ya taifa.

Aidha, amefafanua kwamba mchango wa Barrick katika utafutaji wa madini nchini , umeonekana kwa vitendo kupitia ushirikiano wake na serikali chini ya Wizara ya Madini na Taasisi zake, Barrick imekuwa mdau mkubwa katika shughuli za utafiti za kijiolojia , kutoa ushauri wa kitaalamu, na kuwezeha upatikanaji wa taarifa za kimsingi za madini.
Pamoja na mambo mengine , Dkt. Ngido ameongeza kuwa kwa taarifa za tafiti zisizofaa kwa uchimbaji mkubwa , serikali imekuwa inazitumia taarifa hizo kugawa maeneo kwa ajili wachimbaji wadogo na kuboresha ufanisi wao , sambamba na malengo ya serikali ya kurasimisha na kuendeleza sekta ya uchimbaji mdogo , mfano wa maeneo ambayo tafiti za Barrick zimetumiwa na wachimbaji wadogo , ni Majimoto , Komarera na Golden Ridge ambapo shughuli za wachimbaji wadogo zimekuwa na tija.
“Kwa kipindi cha miaka mitano tayari tumewekeza Shilingi bilioni 100 katika kufanya utafiti wa kisayansi ili kuweza kugundua maeneo mapya kwa ajili ya uwekezaji mkubwa,” amesema Dkt. Ngido.
Kwa upande wake , Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga , Mboni Mhita amesisitiza kuwa serikali ya Mkoa itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji ili waendelee kufanya kazi zao kwa ufanisi ili serikali iendelee kukusanya mapato.
Uzinduzi huo ni sehemu ya uwekezaji endelevu wa Barrick na Twiga katika kuboresha mbinu za utafiti na ugunduzi wa madini , kwa lengo la kupanua wigo wa rasilimali za madini na kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania kwa kizazi cha sasa na kijacho.













Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...