WAZIRI Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, ameitaka jamii kuacha kusubiri matukio makubwa ya viongozi ndipo wajikite kupanda miti, badala yake kufanya zoezi hilo kuwa endelevu kama sehemu ya maisha ya kila siku ili kuisaidia Serikali kutunza na kulinda mazingira nchini.
Pinda amesema hayo leo jijini Dodoma wakati wa zoezi la upandaji wa miti 1,000 katika eneo la Njedengwa,koani Dodoma, lililohusisha Taasisi ya Habari Conservation,wakazi wa eneo hilo pamoja na wanafunzi wa shule mbalimbali.
Amesema jamii haipaswi kusubiri matukio maalumu, kama siku za kuzaliwa za viongozi, ndipo ianzishe kampeni za upandaji miti, bali ihakikishe kuwa tabia ya kupanda na kutunza miti inakuwa endelevu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Wananchi kuanzia ngazi ya kata hadi taifa kwa ujumla, tunapaswa kuwa na utaratibu wa kupanda miti bila kusubiri msukumo kutoka kwa viongozi. Mfano siku ya kuzaliwa ya Rais isiwe ndiyo kigezo pekee, bali tujitume wenyewe kila wakati,” alisema Pinda.
Aliongeza kuwa lengo ni kuona kila Mtanzania anatambua umuhimu wa mazingira kwa kupanda miti ya aina mbalimbali, ikiwemo ile ya kivuli na ya matunda, ili kuchangia kuboresha hali ya hewa na ustawi wa maisha ya jamii.
Aidha, Pinda alimshauri Mkuu wa Mkoa wa Dodoma pamoja na taasisi ya Habari Conservation kutumia vikundi vya vijana, hususan wanaofanya mazoezi ya asubuhi kama kukimbia (mchamchaka), kuwahamasisha kushiriki kampeni za upandaji miti katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema vijana wana nguvu na ushawishi mkubwa katika jamii, hivyo wakitumika ipasavyo wanaweza kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika suala la uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kudhibiti Manunuzi ya Umma (PPRA), Dennis Simba, aliipongeza taasisi ya Habari Conservation kwa kujikita kwenye masuala ya mazingira kwa lengo la kuisaidia serikali kuboresha na kutunza mazingira.
Simba amesema PPRA imeingia makubaliano ya udhamini wa mwaka mmoja na taasisi hiyo, baada ya kujiunga na mfumo wa NesT unaotumika na serikali katika kufanya manunuzi, hivyo wataendelea kushirikiana kuhakikisha miti iliyopandwa katika eneo la Njedengwa na maeneo mengine inatunzwa ipasavyo.
Aliongeza kuwa kwa sasa PPRA imekuwa mdau mkubwa wa mazingira na akaziomba taasisi nyingine kujiunga na mfumo wa NesT ili kwenda kidigitali na kuboresha uwazi katika manunuzi pamoja na kushiriki katika shughuli za kijamii ikiwemo uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alisema mkakati wa mkoa ni kuhakikisha maeneo yote yaliyoainishwa yanapandwa miti kwa ajili ya kutunza mazingira na kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema katika msimu uliopita walifanikiwa kupanda miti 40,000, huku matarajio yao yakiwa ni kuongeza idadi hiyo katika misimu ijayo ili kufikia malengo ya mkoa katika suala la uhifadhi wa mazingira.
Naye mwakilishi wa taasisi ya Habari Conservation, Loyce Obongo, amesema taasisi yao imejipanga kushirikiana na serikali na wadau wengine katika kutekeleza miradi ya upandaji na utunzaji wa miti kwa lengo la kuboresha mazingira na kuhamasisha jamii kuchukua wajibu wao.






.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...