JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linapenda kutoa ufafanuzi wa tukio la kifo cha mtoto Nehemia Cheyo, miaka 13, aliyekuwa Mwanafunzi wa Darasa la Sita katika Shule ya Msingi Kiwira Coal Mine Wilayani Kyela ambaye alipotea na baadae kukutwa amefariki dunia katika Maporomoko ya Mto Lema.
Ni kwamba mnamo Machi 3, 2026 saa 11 jioni katika Kijiji cha Lema kilichopo Kata ya Busale, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Jackson Cheyo, miaka 46, mkazi wa Kijiji cha Lema aligundua kuwa mtoto wake aitwaye Nehemia Cheyo, miaka 13 amekufa maji katika maporomoko ya Mto Lema baada ya kupotea tangu Februari 26, 2026
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia Askari wa kuchunguza matukio ya vifo, lilifika eneo la tukio na kuukuta mwili wa mtoto huyo na kuanza uchunguzi kwa kushirikiana na Daktari kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kyela ambaye alibaini kuwa chanzo cha kifo ni kukosa hewa wakati alipokuwa katika jitihada za kujiokoa ndani ya maji na kupelekea kifo chake.
Katika uchunguzi uliofanywa na Daktari pamoja na Askari wa uchunguzi wa matukio, baba mzazi wa marehemu aitwaye Jackson Cheyo ni miongoni mwa walioshuhudia uchunguzi wa mwili wa mtoto baada ya kumtambua kuwa ni mtoto wake aitwaye Nehemia Cheyo ambaye pia alieleza kuwa Februari 26, 2026 saa 3 asubuhi watoto wake ambao ni Nehemia Cheyo ambaye kwa sasa ni marehemu na Fanikiwa Cheyo walirudi kutoka Shuleni wakidai hakuna masomo kutokana na Walimu kwenda kuhudhuria kikao.
Baba huyo aliendelea kueleza kuwa aliwatuma watoto wake kwenda kuokota maparachichi lakini baada ya nusu saa Fanikiwa Cheyo pekee ndiye aliyerudi na alipoulizwa alidai kuwa kaka yake amepita njia nyingine. Jitihada za kumtafuta zilifanyika lakini hakuonekana hadi Machi 3, 2026 mwili wake ulipokutwa katika eneo ambalo zamani lilikuwa Machimbo ya Makaa ya Mawe lakini kwa sasa kuna maporomoko ya maji ya Mto Lema akiwa amefariki dunia.
Chanzo cha kifo cha mtoto huyo kulingana na uchunguzi na Ushahidi uliokusanywa ni hicho tofauti na taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari zikidai kuwa mtoto huyo aliuawa.
Jeshi la Polisi linamkaribisha yeyote mwenye Ushahidi tofauti na uliokusanywa hadi sasa asisite kuwasilisha.
Imetolewa na:
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...