Na Mwandishi wetu Dodoma
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, leo Mei 07, 2026 amekutana na wananchi wa eneo la Mtumba jijini Dodoma kupitia programu maalum ya “Sema na Waziri” inayoratibiwa na Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Wizara hiyo, kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili wananchi.
Kupitia programu hiyo, wananchi walipata nafasi ya kuwasilisha kero zao moja kwa moja kwa Waziri, kupata ushauri wa kisheria pamoja na kuelekezwa namna sahihi ya kutatua migogoro mbalimbali inayohitaji msaada wa kisheria.
Akizungumza na wananchi hao, Dkt. Homera amesema serikali imejipanga kuhakikisha huduma za kisheria zinasogezwa karibu zaidi na wananchi ili kila Mtanzania aweze kupata haki kwa urahisi bila vikwazo vya kifedha au urasimu.
Amesema bado kuna wananchi wengi wasiokuwa na uwezo wa kugharamia kesi mahakamani au hata kufahamu namna ya kushughulikia changamoto zao za kisheria, hali inayosababisha baadhi yao kuendelea kuathirika bila msaada sahihi.
“Wapo wananchi ambao hawana uwezo wa kifedha wa kwenda mahakamani, lakini pia zipo changamoto ambazo zinahitaji ufafanuzi wa kisheria tu. Zikifika kwetu tunazifanyia kazi na kutoa mwongozo stahiki,” amesema Dkt. Homera.
Aidha, amesema Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kujiimarisha katika utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kuhakikisha kila anayewasilisha changamoto yake anasikilizwa na kupata msaada unaohitajika kwa wakati.
“Sheria ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Ndiyo maana kila mwananchi anayepiga simu au kufika kuwasilisha changamoto yake lazima asikilizwe. Mpaka sasa kupitia programu hii tayari tumeshatatua kero zaidi ya 100 za wananchi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dkt. Homera ametoa rai kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kutatua migogoro kwa njia ya maridhiano badala ya kupeleka kila jambo mahakamani, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa mahabusu na wafungwa magerezani.
“Si kila kesi lazima iende mahakamani. Zingine zinaweza kutatuliwa ndani ya familia au kupitia maridhiano ya kijamii. Hii itasaidia kupunguza migogoro isiyo ya lazima pamoja na msongamano wa watu magerezani,” amesema.
Pia amebainisha kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazowasilishwa mara kwa mara katika programu hiyo ni migogoro ya ardhi na mirathi, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuandika usia mapema wakiwa hai ili kuepusha migogoro ya kifamilia baada ya vifo.
“Changamoto kubwa tunazokutana nazo ni masuala ya ardhi na mirathi. Niwasihi Watanzania kuandika usia mapema wakiwa hai ili kuepusha migogoro inayojitokeza baada ya ndugu kufariki,” amesema.
Programu ya “Sema na Waziri” imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwafikia wananchi moja kwa moja, kusikiliza changamoto zao na kuwapatia msaada wa kisheria kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa haki nchini.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...