Na Pamela Mollel,Arusha 

Maonesho ya kimataifa ya utalii ya KARIBU-KILIFAIR 2026 yanatarajiwa kuifungua Arusha kama kitovu cha sekta ya utalii Afrika Mashariki, huku zaidi ya waoneshaji 550 kutoka mataifa 14 pamoja na mawakala na waendeshaji wa safari zaidi ya 1,000 kutoka nchi zaidi ya 40 wakitarajiwa kushiriki katika tukio hilo litakalofanyika kuanzia Juni 4 hadi 7, 2026 katika viwanja vya Magereza Kisongo mkoani Arusha

Maonesho hayo ambayo yameendelea kujijengea hadhi kama jukwaa kubwa zaidi la utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki, yanatarajiwa kuvutia zaidi ya wageni na wadau wa utalii 15,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani, hatua inayozidi kuthibitisha nafasi ya KARIBU-KILIFAIR kama lango muhimu la biashara na uwekezaji wa utalii barani Afrika

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Wakurugenzi wa Kilifair Promotions, Tom Kunkler na Dominic Shoo, wamesema maonesho hayo yalizaliwa baada ya kuunganishwa kwa maonesho mawili makubwa ya utalii nchini Tanzania ambayo ni KARIBU Fair chini ya TATO pamoja na KILIFAIR ya Kilifair Promotions, muungano ambao umeifanya Tanzania kuwa mwenyeji wa moja ya maonesho yenye ushawishi mkubwa zaidi wa utalii Kusini mwa Jangwa la Sahara

Kwa mujibu wa waandaaji hao, tofauti na miaka iliyopita, maonesho ya mwaka 2026 yatafanyika kwa siku nne kamili huku yakipanuliwa hadi kufikia eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 47,000, hatua inayolenga kutoa nafasi zaidi kwa washiriki, wawekezaji na wadau wa sekta hiyo

Tom Kunkler amesema dhamira yao imeendelea kujengwa katika misingi ya ubunifu, viwango vya kimataifa na mpangilio wa kisasa wa maonesho, huku mwaka huu wakianzisha maeneo mapya ikiwemo “Pan Africa Pavilion” chini ya kampeni ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya “Visit East Africa – Feel the Vibe”, inayolenga kuitangaza Afrika Mashariki kama kitovu cha kipekee cha utalii duniani

Aidha, amesema kaulimbiu ya maonesho hayo ya “Where Business Meets Wildlife” imeendelea kuonesha namna Tanzania ilivyo na nafasi adhimu katika utalii wa mikutano na biashara, ambapo fursa za uwekezaji na biashara zinaenda sambamba na vivutio vya asili, wanyamapori na utamaduni wa kipekee

Waandaaji hao pia wameishukuru Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake katika kukuza sekta ya utalii pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii, Waziri Dkt. Ashatu Kijaji, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), TANAPA na wadau mbalimbali wanaoendelea kushirikiana kuhakikisha maonesho hayo yanakuwa na mafanikio makubwa zaidi kila mwaka

Kwa upande wake Mkuu wa Kanda wa Yas Makao Makuu Dar es Salaam, Robert Sanyagi, amesema ushiriki wa kampuni hiyo katika maonesho ya KARIBU-KILIFAIR 2026 ni sehemu ya mkakati wa kuendelea kusogeza huduma za kidijitali karibu na wadau wa sekta ya utalii pamoja na wananchi kwa ujumla. Amesema maonesho hayo yanatoa fursa muhimu kwa kampuni hiyo kukutana moja kwa moja na wateja wake, kusikiliza mahitaji yao na kuwaonesha teknolojia mpya zinazolenga kuboresha mawasiliano nchini

Sanyagi ameongeza kuwa Yas imejipanga kuonesha uwezo wa teknolojia ya 5G ambayo imeanza kupanuliwa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, hususan ukanda wa Kaskazini ambako shughuli nyingi za utalii hufanyika. Amesema teknolojia hiyo itasaidia kuongeza kasi ya intaneti, kurahisisha mawasiliano ya biashara na kuboresha huduma kwa watalii na wawekezaji wanaoshiriki katika maonesho hayo makubwa ya kimataifa.

KARIBU-KILIFAIR imeendelea kuwa dirisha muhimu la kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia vivutio vyake vya asili na utamaduni vinavyotajwa kuwa miongoni mwa bora duniani. Baadhi ya vivutio hivyo ni pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Bonde la Ngorongoro pamoja na Mlima Kilimanjaro ambao ni mlima mrefu zaidi barani Afrika. Vivutio vingine ni pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na Pori la Akiba la Selous, sambamba na fukwe za kuvutia za Dar es Salaam zinazozidi kuwavutia watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...