KAMPUNI ya mawasiliano ya Airtel Africa imeanza mwaka wake mpya wa fedha wa 2026/27 kwa mafanikio makubwa, baada ya kuongeza mapato kwa asilimia 31 katika robo ya kwanza ya mwaka 2026/27, yakichochewa na kasi kubwa ya matumizi ya intaneti na huduma za kifedha kwa njia ya mtandao.

Akiwasilisha matokeo hayo, Mtendaji Mkuu wa Airtel Africa, Bw. Sunil Taldar, alisema mapato ya kampuni hiyo inayofanya kazi katika nchi 14 barani Afrika, ikiwemo Tanzania, yalifikia dola bilioni 1.853 za Marekani kwa robo mwaka iliyoishia Juni 30, 2026, ikilinganishwa na dola bilioni 1.415 katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Faida baada ya kodi ilipaa kwa asilimia 27 na kufikia dola milioni 198. Kwa kuzingatia viwango vya fedha visivyobadilika (constant currency), mapato ya kampuni yalikua kwa asilimia 21.1, yakionyesha ukuaji thabiti katika huduma za sauti, intaneti na Airtel Money.

Ripoti hiyo inaonyesha ukuaji mkubwa katika maeneo yote makuu ya kibiashara ambapo soko la Nigeria liliongoza kwa kukua kwa asilimia 29.8, likifuatiwa na ukanda wa Afrika ya Kati na Magharibi inayozungumza Kifaransa (Francophone Africa) uliokua kwa asilimia 18, huku ukanda wa Afrika Mashariki ukikua kwa asilimia 17.8.

Ukuaji huo unachochewa na ongezeko kubwa la wateja ambapo katika nchi zote 14, jumla ya wateja wa Airtel iliongezeka kwa asilimia 11.6 hadi kufikia milioni 189.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa asilimia 51 ya wateja wote wa kampuni hiyo sasa wanatumia simu janja (smartphones). Hali hiyo imesababisha idadi ya wateja wa intaneti kuongezeka kwa asilimia 15.5 hadi kufikia milioni 87.3.

Kasi ya matumizi ya intaneti imeongezeka kwa kiwango kikubwa, ambapo wastani wa matumizi ya data kwa mwezi kwa kila mteja ulipaa kutoka Gigabaiti (GB) 7.8 hadi kufikia GB 10.6, na kupelekea matumizi ya intaneti (data traffic) kuongezeka kwa asilimia 56.3 ndani ya mwaka mmoja.

Upande wa huduma za kifedha, wateja wa Airtel Money waliongezeka kwa asilimia 23.3 hadi kufikia milioni 56.5.

Thamani ya miamala inayofanyika kupitia Airtel Money sasa imevuka dola bilioni 245 za Marekani kwa mwaka (ongezeko la asilimia 51.5), huku mapato ya huduma hiyo pekee yakikua kwa asilimia 38.9 na kufikia dola milioni 404.

Ili kuhimili kasi hii ya ukuaji na mahitaji makubwa ya wateja, Airtel Africa imewekeza kiasi cha dola milioni 389 za Marekani katika robo-mwaka hiyo kwa ajili ya kupanua miundombinu yake.

Airtel Africa pia ilifanikiwa kujenga minara na vituo vipya vya mawasiliano zaidi ya 920, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kujengwa katika robo ya kwanza ya mwaka katika historia ya kampuni hiyo, pamoja na kutandaza mtandao wa nyaya za mawasiliano (fibre) hadi urefu wa kilomita 82,100 ili kuimarisha upatikanaji wa huduma bora.

Mapato kabla ya Riba, Kodi, Kushuka kwa Thamani, na Malipo ya Madeni (EBITDA) iliongezeka kwa asilimia 36.6 hadi dola milioni 928, huku kiwango cha faida cha EBITDA kikiboreka hadi asilimia 50.1.

Aidha, fedha taslimu zitokanazo na uendeshaji ziliongezeka kwa asilimia 38.3 hadi dola milioni 786, zikionyesha uimara wa kampuni licha ya kupanda kwa gharama za nishati.

"Tumeanza mwaka huu kwa matokeo mazuri tena. Kuongezeka kwa matumizi ya simu janja, ushiriki mkubwa wa wateja katika huduma za kidijitali na uwekezaji unaoendelea katika miundombinu vinaendelea kuchochea ukuaji wetu," alisema Bw. Taldar.

Katika hatua nyingine ya kimkakati, Bw. Taldar alithibitisha kuwa kampuni hiyo inaendelea na mpango wake wa kuorodhesha biashara ya Airtel Money katika Soko la Hisa la London (London Stock Exchange - LSE), punde tu itakapopata idhini kutoka kwa mamlaka husika, lengo likiwa ni kuongeza thamani ya biashara hiyo na kuvutia wawekezaji wengi zaidi wa kimataifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...