Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limesema litaendelea kutekeleza mkakati wa kuwafikia wananchi kwa kuwapatia taarifa sahihi kuhusu elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili kuongeza uelewa na ushiriki wa wadau katika sekta hiyo.
Hayo ameyasema Meneja wa NACTVET Zanzibar, Elitha Mbedule, wakati akizungumza katika Banda la NACTVET kwenye Maonesho ya Saba (7) ya Wiki ya Elimu ya Juu yanayoendelea katika Viwanja vya Gombani Mpya, Pemba.
Amesema maonesho hayo ni jukwaa muhimu kwa NACTVET kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na baraza hilo, ikiwemo taratibu za kuanzisha vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na usajili na udhibiti wa taasisi hizo.
Aidha, amesema maonesho hayo yanawapa fursa wahitimu wa ngazi ya stashahada wanaotarajia kuendelea na masomo ya elimu ya juu kufika na kupata maelezo ya kina kuhusu udahili, kwa kuwa vyuo vikuu mbalimbali vinashiriki katika maonesho hayo.
"NACTVET itaendelea kutoa elimu kwa wadau wake kuhusu huduma na taarifa mbalimbali zinazohusu elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati," amesema Elitha.
Ameongeza kuwa ushiriki wa NACTVET katika maonesho hayo una lengo la kuhamasisha jamii kutambua mchango wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi katika kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini.


.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...