Na Mwandishi Wetu
TANZANIA inatarajia kuongeza idadi ya wataalamu wazawa wenye ujuzi wa kisasa katika sekta ya madini baada ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuzindua mitaala sita ya mafunzo ya uchimbaji wa madini chini ya ardhi, hatua inayolenga kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika miradi ya madini na kuchochea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza Julai 8, 2026 wakati wa kupokea rasmi mitaala hiyo pamoja na mpango wa utekelezaji wake, Mwenyekiti wa Chemba ya Migodi Tanzania (TCM), Mhandisi Philbert Rweyemamu, alisema sekta ya madini imeendelea kuwa nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia uzalishaji, ajira, mapato ya Serikali na maendeleo ya viwanda.

Alisema maendeleo ya sekta hiyo yanahitaji nguvu kazi yenye ujuzi wa kisasa unaoendana na matumizi ya teknolojia za kisasa katika shughuli za uchimbaji wa madini chini ya ardhi.

Rweyemamu alibainisha kuwa kwa miaka mingi kampuni nyingi za madini zilitegemea kuajiri wataalamu kutoka nje ya nchi kutokana na uhaba wa wataalamu wa Kitanzania wenye ujuzi maalumu, lakini kupitia Mradi wa Mafunzo ya Ufundi wa Madini (IMTT), VETA imeanza kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kufanya kazi katika migodi ya ndani na nje ya Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dkt. Abdallah Ngodu, alisema mitaala hiyo imeandaliwa kwa ushirikiano kati ya VETA, wadau wa sekta ya madini na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), ili kuhakikisha mafunzo yanakidhi mahitaji halisi ya soko la ajira.

Alisema katika hatua ya awali, utekelezaji wa mitaala hiyo utaanza katika Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma Moshi, ambapo kitakuwa kituo cha mwanzo cha kuandaa wataalamu wa uchimbaji wa madini chini ya ardhi.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Migodi Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka, alisema kuanza kwa utekelezaji wa mitaala hiyo kutaimarisha sera ya ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini (Local Content) kwa kuongeza idadi ya wataalamu wazawa na kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi.

Naye Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kaskazini, Monica Mbelle, alisema mitaala hiyo inajumuisha mafunzo ya uendeshaji wa mitambo ya kubeba na kusafirisha miamba migodini, uendeshaji wa mitambo ya kuchimba mahandaki, uendeshaji wa mitambo ya kuchimba mashimo marefu, uendeshaji wa mitambo ya kuchimba mashimo ya ndani ya miamba, maandalizi ya ulipuaji wa miamba chini ya ardhi pamoja na matumizi salama ya vifaa vya kunyanyua na kufunga mizigo.

Uzinduzi wa mitaala hiyo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika sekta ya madini, kuimarisha ushindani wa Watanzania katika soko la ajira na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa taifa.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...