Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kupitia Chuo cha VETA Chang'ombe, imebuni pikipiki ya magurudumu matatu (Bajaj) yenye teknolojia ya kisasa ya kufagia barabara, ubunifu unaolenga kuongeza ufanisi katika usafi wa miji na kupunguza gharama za usafi wa mazingira.
Akizungumza katika Banda la VETA kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es Salaam, Mwalimu wa Chuo cha VETA Chang'ombe, Emmanuel Bukuku, amesema kifaa hicho kina uwezo wa kufagia barabara urefu wa kilomita mbili kwa saa moja.
Bukuku amesema mashine hiyo imeundwa kwa mfumo unaokusanya vumbi, mchanga na taka ndogondogo wakati wa kufagia na kuzipeleka kwenye sehemu maalumu ya kuhifadhi, hivyo kuacha barabara zikiwa safi na salama kwa matumizi.
Ameeleza kuwa ubunifu huo unaweza kuwa suluhisho kwa halmashauri, manispaa na majiji nchini katika kuboresha huduma za usafi wa barabara kwa kutumia teknolojia ya ndani, badala ya kutegemea nguvu kazi kubwa ya watu pekee.
"Teknolojia hii imeundwa na wataalamu wetu wa VETA kwa kuzingatia mahitaji ya mazingira ya Tanzania. Inaongeza ufanisi, inapunguza muda wa kufanya usafi na inaweza kusaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za usafi katika mamlaka za serikali za mitaa," amesema Bukuku.




.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...