Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imeelekeza halmashauri zote nchini kutenga asilimia tano ya mapato yao ya ndani kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya biashara ili kuwawezesha wananchi, hususan vijana na wanawake, kufanya shughuli za kiuchumi katika mazingira bora na yenye tija.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Ingwe Sekondari, Jimbo la Tarime Vijijini, wilayani Tarime, mkoani Mara, leo Jumatano, Julai 1, 2026, Waziri Mkuu alisema hatua hiyo inalenga kuondoa changamoto za maeneo ya biashara na kuongeza fursa za uzalishaji na ajira.
"Tumeenda kuweka asilimia tano kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maeneo ya biashara. Na kwenye hiyo asilimia tano, nimewaelekeza wenzetu wa TAMISEMI kwamba kama kuna eneo vijana wanalitaka kwa ajili ya kufanyia biashara, hata kama hilo eneo lina wamiliki, tumieni asilimia tano kulinunua. Msiwapeleke vijana kufanyia biashara maeneo ya mbali ambayo hayaendani na biashara wanazozifanya."
Aidha, Waziri Mkuu alisema Serikali imepitisha utaratibu wa kuwapa wafanyabiashara wanaoanzisha biashara mpya kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kuanza kulipa kodi, ili kuwapa nafasi ya kuimarisha biashara zao.
"Wale vijana na kina mama wanaoanzisha biashara mpya hawataanza kudaiwa kodi mara wanapoanzisha biashara. Sasa watakuwa na likizo ya mwaka mzima ili wajipange katika kuimarisha biashara zao."
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Serikali itawasilisha bungeni marekebisho ya sheria inayohusu kutaifisha mifugo kwa lengo la kuondoa adhabu ambazo zimekuwa zikiwaathiri wafugaji bila kuathiri juhudi za uhifadhi.
"Bunge lijalo la mwezi wa nane tunaenda kufuta sheria inayotaifisha mifugo ya Watanzania. Tumetathmini tukagundua kwamba sheria hiyo inawatia umaskini Watanzania. Tumegundua katika baadhi ya maeneo adhabu imekuwa kubwa kuliko kosa lililotendwa."
Pia, Waziri Mkuu alisema Serikali imeelekeza kusitishwa kwa utaratibu wa kukamata vitendea kazi vya wananchi kwa madai ya faini, akisema hatua hiyo imekuwa ikikwamisha shughuli za uzalishaji na kujiongezea kipato.
"Kama mtu anadaiwa faini, mwacheni kitendea kazi chake, aendelee kufanya kazi ili awalipe faini. Tuache utekelezaji wa sheria wa kishamba shamba."
Sambamba na hayo, Waziri Mkuu alisisitiza kuwa Serikali haitavumilia ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka katika utumishi wa umma.
"Mtu akiiba, mtumishi wa umma akiiba, msimhamishe. Mfukuzeni kazi. Hatuna uhaba wa watu wa kufanya kazi."
Akihitimisha, Waziri Mkuu aliwataka wananchi kuendelea kulinda amani, umoja na usalama wa nchi, akisisitiza kuwa maendeleo ya taifa na ustawi wa wananchi unategemea kuwepo kwa mazingira ya amani, utulivu na mshikamano.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...