Na Mwandishi Wetu, Dodoma
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amesema Tume ya Ushindani (FCC) ina mchango mkubwa katika kuongeza thamani ya mazao ya Watanzania kupitia utoaji wa elimu kuhusu ushindani wa haki na ulinzi wa mlaji, jambo linalowasaidia wazalishaji na wafanyabiashara kuboresha ubora wa bidhaa zao na kuongeza ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Londo ametoa kauli hiyo leo Agosti 7, 2026, alipotembelea banda la FCC katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.
Amesema elimu inayotolewa na FCC imeendelea kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa ushindani wa haki, ulinzi wa mlaji na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini, hatua inayochochea ukuaji wa biashara na uchumi.
Aidha, ameipongeza FCC kwa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha mazingira ya biashara, akieleza kuwa juhudi hizo zinaendana na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga soko lenye ushindani wa haki, uwazi na fursa sawa kwa wafanyabiashara wote.
Londo ameihimiza FCC kuendelea kutumia Maonesho ya Nanenane pamoja na majukwaa mengine ya elimu ya umma kuwafikia wananchi wengi zaidi ili kuongeza uelewa kuhusu sheria za ushindani na ulinzi wa mlaji.
Amesisitiza kuwa elimu hiyo ni nyenzo muhimu katika kuongeza thamani ya mazao, kuvutia masoko mapya na kuongeza kipato cha wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali.
Pia ametoa wito kwa makundi hayo kutumia ipasavyo elimu wanayoipata kutoka FCC kwa kuboresha uzalishaji, kuzingatia sheria za ushindani na kuepuka vitendo vinavyovuruga soko, akibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kujenga uchumi shindani na kuongeza mchango wa sekta za uzalishaji katika maendeleo ya taifa.



.jpeg)

.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...