📍Taasisi 300 kukaguliwa uzingatiaji wa sheria za utumishi wa umma

Serikali imeanza rasmi Ukaguzi wa Uzingatiaji wa Sheria katika Usimamizi wa Utumishi wa Umma kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027, unaolenga kuhakikisha Taasisi za Serikali zinafuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika usimamizi wa masuala ya kiutumishi na kiutawala.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amebainisha  hayo leo Agosti 10, 2026 Jijini Dar es Salaam, wakati akitoa taarifa kuhusu kuanza kwa ukaguzi huo unaotekelezwa na Tume ya Utumishi wa Umma.

Amesema ukaguzi huo ni utekelezaji wa jukumu la Tume kwa mujibu wa Kifungu cha 12(1)(c) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298, kinachoipa Tume mamlaka ya kufanya ukaguzi kwa lengo la kufuatilia na kutathmini kiwango cha uzingatiaji wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya usimamizi wa masuala ya kiutumishi na kiutawala katika Utumishi wa Umma.

Ameeleza ukaguzi huo unaanza leo, Agosti 10, 2026, na utafanyika katika Taasisi 300 za Serikali, zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa 105, Taasisi za Serikali Kuu 78 na Taasisi za Umma 117, zilizopo katika Mikoa 16 nchini.

Mikoa itakayohusishwa katika ukaguzi huo ni Mwanza, Dodoma, Dar es Salaam, Arusha, Mara, Iringa, Morogoro, Lindi, Simiyu, Kilimanjaro, Shinyanga, Manyara, Songwe, Tanga, Kagera na Geita.

Aidha, Mhe. Ridhiwani amewataka Waajiri katika Taasisi zote zitakazofanyiwa ukaguzi kushirikiana na Tume ya Utumishi wa Umma kwa kutoa ushirikiano na taarifa zinazohitajika ili kuwezesha ukaguzi huo kufanyika kwa ufanisi.

Amesisitiza kuwa ukaguzi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha uwajibikaji, utawala bora na uzingatiaji wa sheria katika Utumishi wa Umma, hatua ambayo itasaidia kuboresha usimamizi wa rasilimali watu na utoaji wa huduma kwa wananchi.














 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...