Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekanusha taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu hali ya baridi nchini, zikidai kuwa kuanzia kesho saa 11:00 alfajiri kwa muda wa saa 27 kutashuhudiwa tukio la Aphelion litakaloambatana na baridi kali kuliko kawaida.

TMA imesema taarifa hiyo ni potofu, huku ikifafanua kuwa tukio la Aphelion ni hali ya kawaida katika mzunguko wa Dunia kwenye mfumo wa Jua (Solar System), inayotokea kila mwaka na kuhusisha Dunia kuwa mbali zaidi na Jua.

Kwa mujibu wa TMA, mchango wa tukio hilo katika mwenendo wa hali ya baridi kati ya msimu mmoja na mwingine ni mdogo sana katika maeneo ya Tanzania kutokana na nchi hiyo kuwa karibu na Ikweta.

TMA imesema kwa kawaida, kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti kila mwaka ni majira ya Kipupwe katika maeneo mengi nchini, ambapo mifumo ya hali ya hewa hutawaliwa na hali ya baridi na upepo mkali.

Aidha, imesema utabiri wa msimu wa Kipupwe uliotolewa Mei 25, 2026 unaonesha kuwa hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo ya Kanda ya Ziwa Victoria, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kusini, Nyanda za Juu Kusini Magharibi pamoja na Mkoa wa Singida.

Kwa mujibu wa utabiri huo, hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini na maeneo ya nchi kavu, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Pwani ya Kusini pamoja na Mkoa wa Dodoma.

TMA imesema vipindi vya baridi zaidi vilitarajiwa kujitokeza mwezi Julai 2026.

Viwango vya joto la chini vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 6°C hadi 21°C katika maeneo ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi, kati ya nyuzi joto 10°C hadi 20°C katika maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, kati ya nyuzi joto 8°C hadi 22°C katika maeneo ya Kanda ya Kusini na kati ya nyuzi joto 10°C hadi 25°C katika maeneo mengine ya nchi yaliyosalia.

TMA imewakumbusha wananchi kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya Mwaka 2019, TMA ndiyo taasisi pekee yenye jukumu na mamlaka ya kutoa taarifa za utabiri na tahadhari za hali ya hewa kwa umma.

Imeeleza kuwa ni kosa kisheria kutoa au kusambaza taarifa zisizo rasmi kwa mujibu wa vifungu vya 27, 31(5) na 46(1) vya Sheria hiyo.

TMA imetoa ufafanuzi huo Dar es Salaam, Agosti 9, 2026, kufuatia taarifa iliyosambaa katika mitandao ya kijamii ikidai kuwa tukio la Aphelion lingesababisha baridi kali kuliko kawaida, hali ambayo ingeweza kusababisha mafua, kikohozi na matatizo ya kupumua.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...