Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Nolasco Kipanda, akifungua mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wakaguzi wa Tume hiyo yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa lengo la kuwajengea uelewa wakaguzi hao wenye jukumu la kukagua uzingatiaji wa sheria na miongozo mbalimbali katika sekta ya umma.
Mkurugenzi wa Mafunzo, Tafiti, Takwimu na Uhamasishaji wa OSHA, Bw. Joshua Matiko, akitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizoibuliwa na washiriki katika mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa Wakaguzi wa Tume ya Utumishi wa Umma yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA).
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Nolasco Kipanda (Katikati) akiwa na viongozi wenzake wakifuatilia mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa na OSHA kwa Wakaguzi wa Tume hiyo.
Meneja Mafunzo wa OSHA, Mhandisi Shaban Mkindi, akiwasilisha mada katika mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa Wakaguzi wa Tume ya Utumishi wa Umma yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA).
Wakaguzi wa Tume ya Utumishi wa Umma wakifuatilia mada mbalimbali katika mafunzo yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa lengo la kuwajengea uelewa juu ya masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.
Afisa Mafunzo Mwandamizi wa OSHA, Bw. Simon Lwaho, akiwasilisha mada katika mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa Wakaguzi wa Tume ya Utumishi wa Umma yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA).

Na Mwandishi Wetu
TUME ya Utumishi wa Umma imesema serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha watumishi wa umma wanakuwa salama na wenye afya njema na hivyo kutekeleza wajibu wao wa kuwahudumia wananchi ipasavyo.

Kauli hiyo imeelezwa na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Nolasco Kipanda, alipofungua mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wakaguzi wa Tume hiyo yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa lengo la kuwajengea uelewa wakaguzi hao wenye jukumu la kukagua uzingatiaji wa sheria na miongozo mbalimbali katika sekta ya umma.

Amesema serikali inatamani kuona kila mtumishi wa umma anakuwa salama dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi ili aweze kutoa mchango wake kikamilifu katika kutekeleza majukumu ya serikali.

“Sote tunafahamu kwamba kinga ni bora kuliko tiba, Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi inaelekeza maeneo yote ya kazi kuwa na mifumo madhubuti ya kuwalinda wafanyakazi dhidi ajali na magonjwa yatokanayo na kazi. Serikali inaamini kwamba watumishi wakiwa na afya njema, utendaji wao utaimarika na tayari ina chombo chake mahsusi cha kusimamia hilo ambacho ni Taasisi ya OSHA,” ameeleza Katibu wa Tume.

Amebainisha kwamba si wajibu wa Tume kusimamia utekelezaji wa Sheria bali Tume hiyo ina jukumu la kuhakikisha waajiri wanatekeleza sheria hiyo pamoja na miongozo mingine inayotolewa na OSHA ili kulinda afya na usalama wa watumishi wa serikali.

“Kutokana na umuhimu wa rasilimali watu, Serikali kupitia Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ilisisitiza Tume kufanya ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria ya usalama na afya mahali pa kazi ili kuhakikisha watumishi wa umma wanafanya kazi katika mazingira bora na hivyo kuwa na ufanisi,” amesisitiza Katibu Kipanda.

Aidha, amewataka wakaguzi wa Tume kuwa na uelewa wa kina kuhusu Sheria ya Usalama na Afya mahali pa kazi ili waweze kufanya tathmini sahihi ya utekelezaji wa sheria hiyo na kushauri maboresho stahiki.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, ameipongeza serikali kwa kudhihirisha nia ya dhati ya kuwalinda watumishi dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi kupitia utekeleza wa sheria na miongozo ya usalama na afya mahali pa kazi.

"Napenda kutoa shukrani zangu kwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuonesha nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba nguvukazi ya nchi inalindwa katika sekta zote za umma na binafsi ambapo kupitia maelekezo yake masuala ya usalama na afya yamejumuishwa katika kanuni za kudumu za utumishi wa umma,” amesema Mwenda na kuongeza:

“Tunaishukuru Tume kwa kutushirikisha ambapo tumeweza kuandaa mafunzo ya kuwajengea uelewa wakaguzi wake ili wakienda kukagua wajue ni maeneo gani muhimu ya kuyafuatilia na wametuahidi baada ya ukaguzi tutakuwa na kikao cha pamoja kwa ajili ya kupata mrejesho.”
Baadhi ya Wakaguzi wa Tume wameyaelezea mafunzo hayo kama nyenzo muhimu katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Mafunzo haya yametupa uelewa mpana sisi kama wakaguzi utakaotuwezesha kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi,” ameeleza Rose Silayo. 

“Kipekee ninashukuru kwa mafunzo haya ambayo yatatuwezesha kukagua na kushauri ipasavyo uzingatiaji wa masuala ya usalama na afya ili kulinda afya za watumishi wa umma,” ameeleza David Shombe.
Mwaka 2022, Tume ilifanya maboresho ya mfumo wa ukaguzi wa masuala ya kiutumishi ili kuendana na sera, sheria na mazingira ya wakati husika ambapo maeneo sita ya kiutawala yaliongezwa katika maeneo saba yaliyokuwa yakikaguliwa awali. Eneo la usalama na afya kazini ni miongoni mwa maeneo yaliyoongezwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...