Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetakiwa kushirikiana na kiwanda cha kutengeneza samani za ndani cha EDOSAMA, kilichopo Kinyerezi, Dar es Salaam, katika kuandaa Watanzania wengi zaidi wenye ujuzi na umahiri katika fani ya useremala ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mohamed Omar, wakati wa ziara katika karakana za kiwanda hicho kwa lengo la kujionea namna shughuli za useremala zinavyoendeshwa pamoja na matumizi ya mashine na teknolojia za kisasa katika utengenezaji wa samani mbalimbali.

Akizungumza na viongozi wa VETA na EDOSAMA wakati wa ziara hiyo, Dkt. Omar amesema moja ya matakwa ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kukuza ushirikiano kati ya waajiri, wenye viwanda na vyuo vya elimu na mafunzo, ili kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaowawezesha kujiajiri, kuajiriwa na kuajiri wengine, sambamba na kukidhi mahitaji ya soko la ajira.

Amesema ushirikiano kati ya VETA na EDOSAMA utakuwa na umuhimu mkubwa katika kuzalisha vijana wenye uwezo na weledi wa kushindana katika soko la ajira, hususan katika sekta ya utengenezaji wa samani.

“Na sisi kama Wizara ya Elimu na wasimamizi wakuu wa mpango huo, tumeona umuhimu wa ushirikiano kati ya VETA yenye jukumu la kuzalisha vijana kupitia utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi na EDOSAMA kama kituo cha uandaaji mafundi mahiri katika eneo la utengenezaji wa samani,” amesema Dkt. Omar.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Kasore, amemshukuru Naibu Katibu Mkuu kwa ziara hiyo na kueleza kuwa Februari 2026, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilizindua mpango wa ushirikiano baina ya waajiri, wenye viwanda na vyuo vinavyotoa elimu na mafunzo ya ufundi stadi.

Amesema mpango huo unalenga kuhakikisha Watanzania, hasa vijana, wanapatiwa ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na hivyo kuchangia kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Jukumu letu VETA ni kuhakikisha tunayaishi maono ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa mafunzo yatakayowapa Watanzania ujuzi na kuwaandaa kushindana katika soko la ajira na kukidhi mahitaji ya wenye viwanda, waajiri na mabadiliko ya teknolojia,” amesema CPA Kasore.

Ameongeza kuwa ushirikiano na EDOSAMA utawezesha kuandaa mitaala inayoendana na mahitaji ya soko la ajira, kuwaandaa wakufunzi wenye uwezo wa kuwapatia vijana ujuzi unaohitajika sokoni, pamoja na kuboresha karakana, mitambo na mashine zinazotumika katika kujifunzia na kufundishia.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa EDOSAMA, Edward Saguda, amesema sekta ya misitu bado ina mchango mdogo katika uchumi wa nchi, ikiwa inachangia asilimia 3.5 ya Pato la Taifa, licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kuongeza mapato na ajira.

Saguda amesema iwapo sekta hiyo itaangaliwa kwa mtazamo mpana zaidi na Serikali, inaweza kuongeza mchango wake hadi zaidi ya asilimia 10 ya mapato ya Serikali na kutengeneza ajira nyingi zaidi kwa Watanzania.

Ameiomba VETA kuharakisha kuanzisha ushirikiano rasmi na EDOSAMA ili kusaidia Serikali na Watanzania kunufaika zaidi na fursa zilizopo katika sekta ya misitu na utengenezaji wa samani




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...