Na Mwandishi Wetu

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Jonas Mpogolo, amezindua rasmi Kampeni ya “Safisha Mazingira, Linda Afya” katika Kata ya Kisutu, huku akimpongeza Diwani wa kata hiyo, Tousif Mohammedali Bhojani, kwa kuwa diwani wa kwanza wilayani humo kuanzisha kampeni hiyo.

Mbali na uzinduzi huo, Diwani Bhojani alimkabidhi Mkuu wa Wilaya vifaa mbalimbali vya usafi vilivyotolewa na wadau kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za usafi na utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wengine, ya kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linakuwa safi.

Uzinduzi huo ulifanyika katika Soko la Baba na Malishe, Kisutu, na kuendelea katika mitaa mbalimbali ya kata hiyo, ukiongozwa na DC Mpogolo akishirikiana na wananchi na wadau wa maendeleo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mpogolo alimpongeza Diwani Bhojani kwa kuwa diwani wa kwanza katika Jimbo na Wilaya ya Ilala kuzindua kampeni hiyo.

Alisema Wilaya ya Ilala ina jumla ya kata 36 na kwamba Kata ya Kisutu, chini ya uongozi wa Diwani Bhojani, imeonesha dhamira ya dhati ya kutekeleza kwa vitendo kampeni hiyo muhimu ya usafi.

Mpogolo alisema wilaya imeandaa mikakati ya kuzishindanisha kata na mitaa yote ya maeneo ya katikati ya jiji (CBD) katika suala la usafi, huku kata na mitaa itakayofanya vizuri ikitarajiwa kupewa zawadi.

“Katika kuhamasisha suala la usafi, tumeandaa zawadi ambazo zitatolewa kwa kata na mitaa ya mjini, yaani CBD, itakayofanya vizuri katika usafi. Lengo ni kuhamasisha kampeni hii ya usafi katika wilaya yetu. Kisutu mmeonesha mfano kwa kuwa kata ya kwanza kuzindua kampeni hii muhimu,” alisema Mpogolo.

Aidha, alisema Wilaya ya Ilala itaendelea kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha usafi unakuwa sehemu ya utamaduni wa wananchi, kuanzia ngazi ya mtu mmoja, familia hadi jamii nzima.

“Tunaenda kutekeleza sheria zetu ndogo kwa wananchi watakaokiuka sheria za usafi. Wale watakaovunja sheria tutawakamata na kuwafikisha katika Mahakama ya Jiji. Akipatikana na hatia atalipishwa faini au kifungo,” alisema.

Aliwataka wananchi wa Kata ya Kisutu na Wilaya ya Ilala kwa ujumla kuhakikisha wanazingatia kanuni za usafi, ikiwemo kuwa na vifaa vya kuhifadhia taka na kufuata sheria na taratibu zinazohusu usafi wa mazingira.

Kwa upande wake, Diwani Bhojani alisema kata hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha inadumisha usafi, ikieleza kuwa usafi hautakuwa shughuli ya Jumamosi pekee au wakati wa kampeni, bali utakuwa sehemu ya maisha ya kila siku.

“Hivi karibuni Rais Dk. Samia alitamka kuwa Jiji ni chafu. Tamko lile lilikuwa ni ujumbe kwetu. Tuko tayari kutekeleza kwa vitendo agizo hilo,” alisema.

Alisema tangu Rais alipotoa kauli hiyo, Kata ya Kisutu imeendelea kufanya usafi na kuwataka wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kushiriki katika kampeni hiyo.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...