MKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kamishna wa Polisi Ramadhani Kingai, amegoma kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi wa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, anayekabiliwa na mashtaka ya uhaini katika Mahakama Kuu Masijala Ndogo Dar es Salaam.
Hatua hiyo imempelekea mshtakiwa Lissu, ambaye anajitetea mwenyewe katika kesi hiyo, kufunga ushahidi wa upande wa utetezi.
Kesi hiyo leo, Septemba 18, 2026, iliitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa upande wa utetezi, ambapo DCI Kingai alitarajiwa kutoa ushahidi.
Akizungumza mbele ya Jopo la Majaji linaloongozwa na Jaji Dustun Ndunguru, Lissu amedai amekutana na DCI Kingai, ambaye alikuwa amependekeza awe shahidi wake wa leo, ndani ya chumba cha mahakama na kuzungumza naye kwa kina kuhusu suala la kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi.
Amedai kuwa baada ya kumweleza Kingai maeneo ambayo angependa ayatolee ushahidi, shahidi huyo alimweleza kuwa hawezi na hayuko tayari kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi.
“Mimi nimemuelewa kama hayuko tayari, siwezi kumlazimisha kutoa ushahidi ambao hayupo tayari kuutoa,” amedai Lissu.
Amedai Kingai amemweleza kuwa yeye yuko upande wa watu wanaoomba na watakaoshangilia endapo atapatikana na hatia, hivyo hayuko tayari kutoa ushahidi kwa niaba yake.
“Yeye yuko upande wa wale wanaoomba na watakaoshangilia nikipatikana na hatia, kwa hiyo amesema hayuko tayari kuja kutoa ushahidi kwa niaba yangu,” amedai Lissu.
Amedai Kingai pia amemweleza kuhusu mashahidi wengine wawili ambao ni Mkuu wa Majeshi, CDF Jacob Nkunda, na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camilius Wambura, ambao pia mahakama iliamuru wapelekewe wito, kuwa nao watakaporejea nchini na kupata wito wa mahakama, msimamo wao utakuwa kama wake.
“Kwamba na wao hawatakuwa tayari kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi, hawawezi kwa sababu ile ile ya wale wanaoombea na watakaoshangilia nikipatikana na hatia,” amedai Lissu.
Kutokana na hali hiyo, Lissu amesema hana mashahidi wengine wa kuwaita na hivyo ameomba kufunga ushahidi wa upande wa utetezi.
Baada ya kusikiliza maelezo hayo, kesi hiyo sasa imefungwa kwa pande zote mbili na kuomba kupangiwa siku ya kuwasilisha hoja za mwisho.
Upande wa utetezi umeeleza kuwa ratiba ya kikao cha mahakama inaishia Septemba 25, hivyo kubaki siku saba za kuandaa hoja za mwisho.
Lissu amesema yuko tayari kuwasilisha hoja hizo Jumatano, huku akieleza kuwa mwenendo wa kesi una hoja zaidi ya kurasa 1,000.
Upande wa Jamhuri umekubaliana na Lissu kuhusu tarehe hiyo na kueleza kuwa utakuwa tayari kwa ajili ya kuwasilisha hoja za mwisho.
Kesi imeahirishwa hadi Septemba 23, 2026.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...