Na Mwandishi wetu, Bulyanhulu - Shinyanga
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeipongeza OSHA na Mgodi wa Bulyanhulu kwa kuwekeza kwenye mifumo ya Usalama na Afya wa wafanyakazi ili kuhakikisha wafanyakazi wanalindwa dhidi ya vihatarishi na wanapata huduma stahiki wanapopata ajali au changamoto za kiafya kazini.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hawa Chakoma, wakati wa ziara ya kamati katika eneo la mgodi wa Bulyanhulu mkoani Shinyanga, iliyolenga kufuatilia utekelezaji wa sheria namba 297 ya mwaka 2023 inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, kuhusu Usalama na Afya mahali pa kazi.
Mhe. Chakoma amesema kamati hiyo imefanya ziara hiyo ili kutathmini namna wafanyakazi wanavyolindwa dhidi ya vihatarishi vinavyotokana na shughuli za uchimbaji wa madini, pamoja na namna mifumo ya kuwasaidia wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kudhibiti ajali au magonjwa wakiwa kazini.
“Tunataka kuona ni kwa namna gani wenzetu wa mgodi wanajaribu kuondoa vihatarishi kwa wafanyakazi, au kuwahudumia wanaopata changamoto hizo wakiwa mahali pa kazi,” amesema Bi. Chakoma.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Wilbard Munisi, amesema kuwa Serikali kupitia OSHA imeendelea kufanya kaguzi na kutoa elimu ya Usalama na Afya mahali pa Kazi kwa wafanyakazi.
Naibu waziri, Dkt. Munisi amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, jumla ya kaguzi 871 zilifanyika mkoani Shinyanga, huku wafanyakazi 7,969 wakifanyiwa vipimo vya afya mkoani humo.
Aidha, Naibu waziri amesema kuwa waajiri 102 walikidhi matakwa ya sheria ya Usalama na Afya na kupatiwa vyeti vya ithibati, huku waajiri wengine wakipewa maelekezo ya kufanya maboresho katika maeneo yaliyobainika kuwa na changamoto.
Katika eneo la mafunzo, Dkt. Munisi amesema jumla ya wafanyakazi 931 walipatiwa mafunzo kuhusu usalama na afya mahali pa kazi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, kuwa amesema kuwa OSHA inaendelea kusimamia usalama na afya mahali pa kazi kwa kuhakikisha waajiri wanaweka mifumo inayolinda usalama na afya za wafanyakazi huku ikiweka mkazo katika elimu na uhamasishaji ili waajiri waweze kutekeleza wajibu wao kwa uelewa.
Ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati ya Bunge na kufuatilia utekelezaji wa sheria pamoja na maelekezo yaliyowahi kutolewa kuhusu uboreshaji wa usalama na afya mahali pa kazi.



.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...