Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, amesema miradi inayotekelezwa kwa fedha za umma inapaswa kwenda kwa kasi na kuzingatia ubora unaostahili ili wananchi wanufaike na uwekezaji unaofanywa na Serikali.
Kihongosi ametoa kauli hiyo leo, Septemba 19, 2026, baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Barabara za Masuliza na Kilimahewa–Tuangoma katika Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Amesema hajaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara hizo na kusisitiza kuwa mkandarasi anayeshindwa kutekeleza kazi kwa kiwango kinachokubalika anapaswa kuchukuliwa hatua.
“Kama mkandarasi analeta mambo yasiyofaa, achukuliwe hatua na aelezwe kwamba Chama hakijaridhishwa na namna anavyofanya kazi zake katika kutengeneza hii miradi,” amesema Kihongosi.
Amesema CCM na Serikali hazitaruhusu uzembe katika utekelezaji wa miradi inayogharamiwa na fedha za umma, kwa kuwa wananchi wanatarajia kuona matokeo yenye tija kwao na kwa Taifa kwa ujumla.
Kihongosi amesisitiza kuwa msimamo huo unaendana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha miradi ya maendeleo, hususan miundombinu, inatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya ubora na kwa wakati.
Barabara hizo zinajengwa chini ya Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II), ambapo Barabara ya Masuliza ina urefu wa kilomita 4.04, huku Kilimahewa–Tuangoma ikiwa na urefu wa kilomita 7.3.
Ujenzi wa barabara hizo unatekelezwa na GroupSix International Ltd kwa gharama ya Sh bilioni 25.99.
Kwa mujibu wa taarifa ya DMDP II, Wilaya ya Temeke imepangiwa kutekeleza ujenzi wa barabara 42 zenye jumla ya urefu wa kilomita 55.449, zilizogawanywa katika mafungu saba na kusimamiwa na wakandarasi mbalimbali.
Mikataba ya mafungu manne ya kwanza, yenye jumla ya kilomita 32.8, ina thamani ya Sh bilioni 97.17 na utekelezaji wake unaendelea, wakati mafungu matatu yaliyosalia yako katika hatua ya usanifu.
Kupitia DMDP II, Serikali inalenga kuboresha miundombinu ya barabara pamoja na huduma nyingine muhimu katika Manispaa ya Temeke, kwa lengo la kuboresha mazingira ya maisha na shughuli za kiuchumi kwa wananchi.


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...