Na Mwandishi wetu, Nzega
MWENGE wa uhuru umezindua mradi wa Nkuba hotel (Pride of Nzega) iliyopo mjini Nzega Mkoani Tabora wenye thamani ya shilingi 274,000,000.
Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mhe Naitapwaki Tukai akizungumza mbele ya kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2026 Wazo Michael Mwang'onda amesema wanampongeza mmiliki wa hoteli hiyo Ndongo Mabula kwa uwekezaji huo.
Amesema mradi huo ni ishara ya sekta binafsi kuunga mkono juhudi za Serikali kukuza uchumi, kuvutia wageni, kuongeza matumizi yenye tija ya ardhi na kutoa ajira kwa wananchi.
"Mradi huu utaboresha mazingira ya upatikanaji wa huduma za hoteli na ukumbi wa kisasa wa mji wa Nzega, wageni watapata sehemu ya kupumzika na halmashauri ya mji itapata kodi," amesema DC Tukai.
Edina Eliberatus akisoma taarifa ya ujenzi kwa niaba ya mmiliki wa hoteli hiyo Ndongo Mabula amesema ujenzi wa mradi ulianza rasmi Machi mosi mwaka 2025 na kukamilika Septemba 4 mwaka 2026.
Amesema gharama za mradi huo wa hoteli ni shilingi 24,000,000 unahusisha vyumba 12 vya kulala wageni na ukumbi mmoja wa mikutano.
"Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Rais DKt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwa sekta binafsi," amesema Mabula.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2026 Wazo Michael Mwang'onda amempongeza mwekezaji wa hoteli hiyo Ndongo Mabula kwa ujenzi wa mradi huo.
Mwang'onda amesema mwekezaji amejenga bila kuwekewa mikwamo hivyo Serikali ya Wilaya ya Nzega inastahili pongezi kubwa.
"Mwekezaji anapotaka kuwekeza mradi asiwekewe mikwamo na vikwazo wapeni kipaumbele kwani hata Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza sekta binafsi kupewa kipaumbele hivyo Nzega hongereni sana," amesema



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...