Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SHULE ya Mivinjeni Pre and Primary School inatarajia kuanzisha masomo ya lugha ya Kichina na Kiarabu kuanzia mwaka ujao, ikiwa ni hatua inayolenga kupanua wigo wa ujuzi wa lugha kwa wanafunzi na kuwaandaa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira.

Akizungumza katika mahafali ya 26 ya shule hiyo, Mkuu wa Shule ya Mivinjeni Pre and Primary School, Sabas Rweichumu, alisema kuanzishwa kwa masomo hayo ni sehemu ya jitihada za kuwapa wanafunzi maarifa na ujuzi utakaowasaidia katika safari yao ya elimu na maisha kwa ujumla.

Alisema lugha ya Kichina imepewa kipaumbele kutokana na kuwepo kwa fursa mbalimbali zinazohitaji ujuzi wa lugha hiyo, huku Kiarabu kikitarajiwa kuongeza uwezo wa wanafunzi kujifunza na kutumia lugha zaidi ya moja.

Katika mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 55 walihitimu elimu ya msingi, huku Rweichumu akieleza kuwa hayo ni mahafali ya kwanza kufanyika tangu shule hiyo ianze kutumia mtaala wa Kiingereza.

Akizungumza katika hafla hiyo, mgeni rasmi na mdau wa masuala ya maendeleo, Chacha Chogocho, aliwataka wazazi na walezi kuendelea kuwapatia watoto wao elimu, malezi na ulinzi wa kutosha, hasa katika kipindi hiki ambacho wengi wao wanamaliza Darasa la Saba na kusubiri matokeo.

Chogocho aliwataka wanafunzi hao kutumia maarifa waliyopata kutoka kwa walimu wao katika kukabiliana na changamoto mbalimbali watakazokutana nazo wakiwa nyumbani wakati wakisubiri matokeo.

Pia, aliwataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao kutokana na maendeleo ya teknolojia na utandawazi, akisisitiza umuhimu wa kuwaongoza katika matumizi sahihi ya taarifa na maarifa wanayopata.

Aidha, aliwataka wazazi na wananchi wenye uwezo kuwasaidia watoto na watu wengine wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo katika sekta za elimu, afya na miundombinu, ili kujenga jamii yenye usawa na mshikamano.

Akizungumzia historia ya shule hiyo, Chogocho alisema ilianzishwa mwaka 2001 baada ya kutokea Shule ya Msingi Kurasini, kufuatia ongezeko la idadi ya wanafunzi na changamoto ya umbali wa kufuata huduma za elimu katika eneo hilo.

Alisema mwaka 2006 shule hiyo ilikumbwa na mafuriko yaliyosababisha baadhi ya wanafunzi kuhama na kubaki na wanafunzi wasiopungua 100. Hata hivyo, uongozi wa shule pamoja na wazazi waliendelea kushikamana na kukabiliana na changamoto hizo.

Alisema kutokana na jitihada hizo, shule hiyo imeendelea kukua na sasa inapokea wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam, huku ikitajwa kuvutia wazazi kutokana na elimu inayotolewa kwa ada nafuu.

Naye Diwani wa Kata ya Miburani, Hassan Mkenga, alisema viongozi kwa kushirikiana na halmashauri wataendelea kuboresha miundombinu mbalimbali, ikiwemo ya elimu, afya na barabara, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi na wanafunzi.

Alisema kwa sasa kuna ujenzi wa shule nyingine ambao umefikia hatua za mwisho za kukamilika, na kukamilika kwake kutasaidia kuongeza idadi ya shule za serikali pamoja na kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule za kata. 


Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...