Wananchi wa Mkoa wa Pwani wanaendelea kunufaika na ushirikiano kati ya Serikali ya Mkoa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), unaolenga kuimarisha upatikanaji wa Majisafi na salama katika kipindi ambacho Mkoa unakuwa kwa kasi kiuchumi na kiviwanda.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesema Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo DAWASA kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa uhakika na endelevu, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda miundombinu ya maji.

Nyongo ameyasema hayo leo, Septemba 21, 2026, alipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Bodi ya DAWASA ofisini kwake ulioongozwa na Mwenyekiti wa Bodi Mhandisi Romanus Mwangingo.

Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amesema DAWASA inahudumia zaidi ya watu milioni nane katika Mkoa wa Dar es Salaam na baadhi ya maeneo katika Mkoa wa Pwani.

Amesema kwa upande wa Pwani, DAWASA inahudumia takribani watu milioni 1.4, sawa na asilimia 68 ya wakazi wa Mkoa huo, huku mahitaji ya maji yakiongezeka kutokana na kasi ya ukuaji wa viwanda na shughuli nyingine za kiuchumi.

Mhandisi Bwire amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana DAWASA inakabiliwa na changamoto ikiwemo kuongezeka kwa gharama za uendeshaji, madeni kutoka kwa baadhi ya taasisi na upotevu wa Maji hali inayohitaji ushirikiano wa pamoja wa Serikali, Wananchi na wadau wengine.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Nyongo amesema Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana na DAWASA katika kulinda miundombinu na mitambo ya uzalishaji na usambazaji maji, ikiwemo Ruvu Juu, Ruvu Chini na Wami, ili kuepusha uharibifu unaoweza kuathiri huduma.

Amesema ushirikiano huo ni muhimu kutokana na ukuaji wa Pwani katika sekta za kiuchumi, kijamii na viwanda, unaoongeza mahitaji ya maji sasa na katika miaka ijayo.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...