Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

WILAYA ya Rufiji mkoani Pwani imebainika kuwa katika hatari kubwa ya kukumbwa na mafuriko kwa kiwango cha asilimia 75, huku Mkoa wa Pwani ukikadiria zaidi ya Sh bilioni 32.6 zitahitajika kwa ajili ya maandalizi na kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha kuanzia Oktoba mwaka huu hadi Januari 2027.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesema kati ya fedha hizo, takribani Sh bilioni 17 zinahitajika kwa ajili ya Wilaya ya Rufiji, ambayo imekuwa ikikumbwa na mafuriko kutokana na historia na jiografia yake, ikiwemo athari zilizojitokeza katika msimu wa mvua wa mwaka 2023/2024.

Akizungumza katika kikao cha wadau wa maendeleo, wakiwemo wawekezaji na viongozi mbalimbali mkoani Pwani, Nyongo amesema pamoja na Rufiji, maeneo mengine yaliyo katika hatari ya kukumbwa na athari za mafuriko ni Bagamoyo, Kibiti na Kisiwa cha Mafia.

“Rufiji lipo kwenye hatari kubwa ya uhatarishi. Mkoa una mahitaji ya zaidi ya Sh bilioni 32.6 kwa ajili ya kukabiliana na hali hiyo ikitokea. Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 17 zinaelekezwa wilayani Rufiji kwa ajili ya kukabiliana na athari zitakazojitokeza na tahadhari,” amesema Nyongo.

Kutokana na hali hiyo, Nyongo amewaagiza wakuu wa wilaya kufanya maandalizi ya mapema na tathmini za mara kwa mara katika maeneo yao ili kubaini maeneo yenye uhatarishi na kuchukua hatua stahiki kabla ya mvua hizo kuanza.

Aidha, amewataka wakuu hao kuratibu na kupokea vifaa pamoja na bidhaa mbalimbali kutoka kwa wadau, wakiwemo wawekezaji, ambao wameonyesha utayari wa kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na maafa endapo yatatokea.

Amesema baadhi ya wadau wameonyesha utayari wa kuchangia vifaa vya uokoaji, magodoro, vyakula, vinywaji na mahema, huku akizitaka halmashauri zote kujiandaa pia kwa kutenga bajeti za dharura.

Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Mipango na Uratibu, Romwald Mwendi, amesema maeneo 14 ya barabara kuu yametambuliwa na tayari yamegawanywa katika zoni nne kwa ajili ya kurahisisha ufuatiliaji na kuchukua hatua za kukabiliana na athari za mvua.

Mwendi amesema maeneo hayo yanahusisha Mkuranga, Vigwaza, Makofia na Msata, ambapo maandalizi yamefanyika kwa kuweka vifaa, ikiwemo makaravati yenye urefu wa mita 500 na vikapu 300, vyenye thamani ya takribani Sh bilioni 12.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Luteni Kanali Fredrick Komba, amesema wilaya hiyo ni miongoni mwa maeneo yenye historia ya kukumbwa na mafuriko, hasa katika msimu wa mvua wa mwaka 2023/2024.

Komba amesema kutokana na tahadhari iliyotolewa kuhusu mvua za El Niño, wataalamu wameandaa mpango kazi unaohusisha hatua za kuzuia athari, maandalizi na uhamasishaji wa wananchi.

Amesema miongoni mwa hatua hizo ni kufanya siku saba za usafi wa kina kwa kushirikiana na wadau na wananchi, kufanya ukaguzi wa maeneo yenye uhatarishi pamoja na kuandaa mkutano maalumu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa.

Amebainisha kuwa maeneo ambayo tayari yameonekana kuwa katika hatari zaidi ni Muhoro, Umwe, Shela, Ikwiriri na Chumbi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo, amesema kutokana na Mafia kuwa kisiwa, kata zote za wilaya hiyo zipo katika uhatarishi wa athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.

Amesema Serikali wilayani humo imeendelea kuchukua hatua za maandalizi ili kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Mstaafu Joseph Kolombo, amesema wilaya hiyo imebaini maeneo hatarishi nane yenye jumla ya kaya 5,489 na shule 12, katika kata sita zilizopo Delta ambazo zina historia ya kukumbwa na mafuriko.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...