Na Janeth Raphael MichuziTv 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Clement Sangu (Mb.), amewataka viongozi na wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa Chama hicho unaendeshwa kwa kuzingatia Katiba, misingi ya demokrasia, uwazi, haki, usawa na amani.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa TALGWU uliofanyika Jijini Dodoma, tarehe 17 Septemba 2026, Sangu amesema uchaguzi huo ni sehemu muhimu ya uhai wa Chama na unawapa wanachama fursa ya kuchagua viongozi watakaowaongoza katika kutekeleza majukumu na malengo ya TALGWU.

Sangu amewataka wajumbe kushiriki mchakato wa uchaguzi kwa utulivu na kuheshimiana, akisisitiza kuwa uchaguzi haupaswi kuwa chanzo cha mgawanyiko, bali utumike kama fursa ya kuimarisha umoja na mshikamano wa wanachama. Alieleza kuwa baada ya matokeo kutangazwa, viongozi na wanachama wote wanapaswa kuendelea kushirikiana, kwa kutambua kuwa maslahi ya wafanyakazi ndiyo yanayopaswa kuwa ajenda ya pamoja.

Aidha, Waziri Sangu amesisitiza kuwa Serikali inatambua na kuheshimu uhuru wa vyama vya wafanyakazi, huku akieleza kuwa uhuru huo unaenda sambamba na wajibu wa kuzingatia sheria, Katiba za vyama, uwazi, utawala bora, nidhamu na uwajibikaji. Alisema Serikali inatarajia TALGWU kuendelea kuwa mfano katika uendeshaji wa shughuli zake kwa kuzingatia misingi hiyo.

Waziri huyo pia ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kushirikiana na TALGWU pamoja na vyama vingine vya wafanyakazi kupitia Mfumo wa Majadiliano ya Pamoja (Social Dialogue), ambapo kero, ushauri na mapendekezo ya wafanyakazi yataendelea kupokelewa na kujadiliwa kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya wafanyakazi kwa mujibu wa sheria. Aliongeza kuwa changamoto za wafanyakazi zinapaswa kutatuliwa kupitia majadiliano, mashauriano na taratibu zilizowekwa kisheria.

Kwa upande mwingine, Sangu aliwataka viongozi watakaochaguliwa kuzingatia uadilifu, uwazi, uwajibikaji na maslahi ya wanachama katika kutekeleza majukumu yao, huku akiwahimiza wanachama kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa weledi, nidhamu na uzalendo. Pia aliwapongeza viongozi na wanachama wa TALGWU kwa mchango wao katika kuimarisha umoja wa wafanyakazi, kutatua changamoto na kuchangia maendeleo ya Chama.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...