Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mdau wa maendeleo, Elia Kitomo, ametoa msaada wa fedha na vifaa kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika Shule ya Msingi Ibogo, iliyopo Kijiji cha Magubike, Kata ya Nzihi, pamoja na kusaidia familia yenye uhitaji katika kijiji hicho.

Kitomo ametoa msaada huo alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya Darasa la Sita ya shule hiyo, ambapo alikabidhi Shilingi 500,000 kwa ajili ya ununuzi wa pampu ya kuvuta na kusambaza maji, bomba la maji aina ya poly pipe lenye thamani ya Shilingi 185,000, pamoja na mifuko 20 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mwalimu.

Katika kuunga mkono wananchi wenye uhitaji, Kitomo pia ametoa Shilingi 50,000 kwa ajili ya ukarabati wa nyumba ya familia moja inayokabiliwa na changamoto za maisha katika Kijiji cha Magubike.

Akizungumza katika mahafali hayo, Kitomo amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanaohitimu elimu ya msingi wanaendelea na masomo ya sekondari, badala ya kuwaacha kwenda kuishi kwa ndugu bila mipango madhubuti ya kuhakikisha wanaendelea na elimu.

Ameshauri wazazi kuwaandaa watoto wao kujiunga na mafunzo ya maandalizi ya kuanza elimu ya sekondari (Pre-Form One), akieleza kuwa hatua hiyo itawasaidia kujiandaa vizuri na kukabiliana na changamoto za masomo katika hatua inayofuata.

Alionya kuwa baadhi ya watoto wanaopelekwa kuishi kwa ndugu bila uangalizi wa kutosha wanaweza kukumbana na mazingira yanayohatarisha usalama wao, ikiwemo ukatili na kulazimishwa kufanya kazi za nyumbani badala ya kuendelea na masomo.

Aidha, amewahimiza wazazi kupanga vipaumbele vya familia na kutumia rasilimali walizonazo kwa busara, akisisitiza kuwa elimu ya watoto inapaswa kupewa kipaumbele katika mipango ya maendeleo ya kaya.

Katika hatua nyingine, Kitomo amepongeza uongozi wa Shule ya Msingi Ibogo, walimu, wazazi na wadau wa elimu kwa juhudi zao za kuendeleza shule hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya shule, familia na jamii katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuinua kiwango cha elimu.

Amesema kuwa uwekezaji katika elimu na kusaidia wananchi wenye uhitaji ni sehemu muhimu ya juhudi za kujenga jamii yenye fursa bora za maendeleo na maisha yenye ustawi.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...